UHASAMA wa kisiasa kati ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na watoto, Sophia Simba na Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, umevuka mipaka na sasa ni uadui wa wazi wazi. Hali hiyo ilidhihirika wiki iliyopita mjini Dodoma, wakati wawili hao walipokutana katika Benki ya CRDB iliyopo bungeni na badala ya kusalimiana, waliishia kutofautiana.
Shuhuda wa tukio hilo, aliiambia MTANZANIA, kuwa tukio hilo lilitokea saa 6 mchana, baada ya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuahirisha Bunge kutokana na vurugu zilizosababishwa na wabunge wa upinzani, wakati wa mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Shuhuda huyo alisema kuwa, kabla ya tukio hilo, Anne Kilango pamoja na wabunge wengine wa CCM, walikuwa ndani ya benki hiyo wakibadilishana mawazo.
Wakati wakiendelea kuzungumza, Sophia Simba aliingia ndani na kuanza kuwasalimia kila mmoja kama ilivyo kawaida.
“Sisi tulikuwa hapa ndani ya benki pamoja na Diana Chilolo (Mbunge wa Viti Maalum CCM), Turky, Mbunge wa Mpendae (Salim Abdallah Turky) pamoja na wahudumu wa benki.
“Sofia Simba alipofika, alitusalimia lakini Anne Kilango hakuitikia salamu yake na hapo Sofia akasema, mheshimiwa Anne Kilango nakusalimia.
“Aliposema hivyo tu, Anne Kilango akahamaki na kusema usinisalimie, mimi sitaki salamu yako. Kauli hiyo ilionekana kutushangaza na wakati tunashangaa, Sofia Simba akasema, mheshimiwa Anne Kilango mimi ni shoga yako na tumetoka mbali, kwa nini tusisalimiane?
“Aliposema hivyo, Anne Kilango akasema sitaki kusikia salamu yako, ‘shut up’ kisha akaondoka,” alisema shuhuda huyo akinukuu maneno ya Anne Kilango.
Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo kwa njia ya simu, Simba alisema kwa kifupi, kwamba, “nina ngozi ngumu, sizungumzi mambo haya kwa sababu mimi ni kiongozi,” alisema na kukata simu.
Naye, Anne Kilango alipoulizwa naye alisema yeye hawezi kuzungumzia masuala hayo, kisha akakata simu.
0 maoni:
Chapisha Maoni