Van Persie aipa Ubingwa wa 20 Man United
Van Persie alifunga mabao yote matatu ndani ya dakika 31 za kipindi cha kwanza katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Old Traford na kuwafanya United kufikisha pointi tofauti ya 16 na waliokuwa mabingwa watetezi majirani zao Manchester City,huku wakiwa na michezo minne kibindoni.
Mkongwe Ryan Giggs alianza kwa kumtengenezea nafasi ya goli la kwanza Van Persie dakika mbili baada ya mchezo kuanza kabla ya Wayne Rooney kumpa nafasi nyingine nzuri Van Persie dakika ya 13 na kufunga moja kati ya mabao bora kabisa msimu huu kwa mguu wake wa kushoto na kufanya United kuwa mbele kwa mabao mawili ndani ya dakika 15 za kwanza za mchezo.
Alikuwa ni Giggs kwa mara nyingine aliyempa pande Van Persie na kufunga bao la tatu dakika ya 33 ya kipindi cha kwanza na kufanya uwanja wa Old Traford kulipuka kwa shangwe za mashabiki,kwani ilikuwa dhahiri wamekwisha jihakikisha ubingwa msimu huu.
Hii imekuwa mara ya nne kwa Manchester United kutwaa ubingwa wa ligi kuu soka nchini Uingereza kwenye uwanja wa Old Traford,baada ya kufanya hivyo mwaka 1999,2002 na 2009. Mara ya mwisho United kutwaa ubingwa wa ligi kuu huku wakiwa na michezo mingi iliyosalia ilikuwa mwaka 2001 baada ya kutangazwa mabingwa huku wakiwa na michezo mitano kibindoni.
Kwa matokeo hayo Aston Villa watasalia kwenye nafasi ya 17 wakiwa na pointi zaidi ya timu ambazo zipo kwenye hatihati ya kuteremka daraja.
Manchester United wikiendi ijayo watapambana na Arsenal kwenye uwanja wa Emirates wakati wakisubiri kukabidhiwa kombe lao la ligi kuu katika mchezo wao mwisho kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Old Traford hapo May 12 watakapokuwa wakicheza na Swansea.
0 maoni:
Chapisha Maoni