Ijumaa, 3 Mei 2013

Hukumu ya Ponda wiki ijayo



Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini imepanga Mei 9 mwaka huu, kuwa siku ya hukumu ya kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49.

Katika kesi hiyo, Sheikh Ponda na wenzake wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh 59.6 milioni, uchochezi na kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali.

Jana kesi hiyo ilitajwa tena wakati ikisubiri tarehe ya hukumu.
Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa alisema hukumu dhidi ya Ponda na wenzake itatolewa Mei 9, mwaka huu.

Kama kawaida, Sheikh Ponda na mwenzake Sheik Swalehe Mukadam walifikishwa mahakamani asubuhi wakiwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi na Magereza.

Mapema Hakimu Nongwa baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 17 wa upande wa mashtaka, aliwaona Sheikh Ponda na wenzake kuwa wana kesi ya kujibu katika mashtaka yanayowakabili.

Alitoa nafasi kwa washtakiwa kujitetea na walifanya hivyo.
Wakati kwesi hiyo ikitajwa kwa mara ya kwanza, Wakili wa Serikali, Leonard Challo aliiambia Mahakama kuwa Ponda na Mukadam wanakabiliwa na shtaka la uchochezi.

Alidai kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu katika eneo la Chang’ombe Markazi, wakiwa kama viongozi wa Taasisi na Jumuiya za Kiislamu Tanzania, waliwashawishi wafuasi wao kutenda makosa hayo.

Inadaiwa kuwa siku ya tukio, Sheikh Ponda na wenzake walivamia ardhi inayomilikiwa na Kampuni ya Agritanza Ltd kwa nia ya kujimilisha isivyo halali.

Ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 21 na 16, mwaka huu katika eneo hilo hilo, washtakiwa walijimilikisha ardhi ambayo ni mali halali ya Kampuni ya Agritanza Ltd.

Pia ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu huko Chang’ombe Markazi washtakiwa waliiba vifaa na malighafi mbalimbali za ujenzi, yakiwamo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh 59,650,000 mali ya Kampuni ya Agritanza Ltd. E&P
CHANZO: Mwananchi

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More