Dodoma. Kambi ya Upinzani Bungeni imetoa tuhuma nzito kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ikidai kuwa anajihusisha na mtandao wa ujangili nchini.
Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi amejibu tuhuma hiyo akisema ni za uongo huku akiituhumu kambi hiyo kuwa imedanganya wakati inajua ukweli kuhusu tuhuma dhidi ya Kinana.
Akiwasilisha maoni ya upinzani kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2013/14, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Maliasili, Mchungaji Peter Msigwa alisema vitendo vya ujangili vimekuwa vikilitia doa taifa kwenye jumuiya za kimataifa.
“Kwa bahati mbaya ni kwamba wahusika wengi ambao wanatajwa kwa ushahidi ni makada maarufu na wengine ni viongozi waandamizi wa CCM,” alisema Mchungaji Msigwa.
“Tumeshuhudia watuhumiwa wengine wa ujangili ambao Ikulu imediriki kuwapatia nafasi kubwa za uongozi wa taifa hili, licha ya kutajwa kwenye ripoti ya uchunguzi kuhusiana na ujangili.”
Alisema mwaka 2009, meli ya Kampuni ya Wakala wa Meli ya Sharaf Shipping inayomilikiwa na Kinana ilikamatwa China ikiwa na makontena yenye nyara za Serikali ikiyasafirisha kwenda Hong Kong.
“Nyaraka zilizopo Ofisi za Wakala wa Usajili wa Kampuni na Biashara (Brela), zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ya Kinana ilisajiliwa Oktoba 2003 na kupewa hati na. 47221.
“Nyaraka zinaonyesha kuwa Kinana anamiliki hisa 7,500 kati ya 10,000 za kampuni hiyo iliyosajiliwa Dar es Salaam. Mshirika mwenzake katika kampuni hiyo, Rahma Hussein ambaye ni mke wake anamiliki hisa 2,500,” alisema Msigwa.
Dk Nchimbi ajibu mapigo
Akijibu tuhuma hizo, Waziri Nchimbi alisema: “Ukiona mtu anasimama na kuamua kusema kuwa hakuna kinachofanywa na wizara kuhusu masuala ya ujangili, ni wazi uelewa wake unakuwa na utata mkubwa.”
Alisema hoja zilizojengwa dhidi ya Kinana ni uongo mtupu... “Nimejaribu kufuatilia kwa makini alichokisema alikimaanisha, alikielewa, alikitafakari au aliandikiwa tu akaenda kusoma? Baada ya kutafakari kwa kina nikagundua hakuwa na nia mbaya, aliandikiwa tu na ameenda kusoma,” alisema Dk Nchimbi.
Alisema ukweli wa jambo hilo ni kwamba ipo tofauti ya majukumu ya kampuni za Wakala wa Meli na shughuli za kupakia mizigo bandarini huku akituhumu kambi ya upinzani kuwa inajua ukweli lakini imeamua kupotosha umma.
Dk Nchimbi ambaye alikuwa mchangiaji wa kwanza, alisema wakala hawezi kuwa mmiliki wa meli, bali anamwakilisha mwenye meli kwenye shughuli ndogondogo zinazofanyika inapofika nchi fulani kama kuhudumia watumishi wa meli, mahitaji muhimu na kufanya usafi.
“Lakini kuna watu wanaitwa ‘clearing and forwarding (Kupakua na kupeleka mizigo). Napenda kukwambia Mchungaji Msigwa kuwa kazi yao ni kupeleka na kutoa mizigo bandarini,” alisema Dk Nchimbi na kuongeza;
“Kule ndiko kuna utaratibu wa upekuzi, katika utaratibu wa upekuzi mtu wa ‘shipping agency’ (wakala wa meli) hahusiki, sina shaka hata kidogo Mchungaji Msigwa analijua hili ninalolisema, ila amelifumbia macho kwa makusudi kwa masilahi yasiyokubalika katika taifa.”
Alisema kumekuwa na uvumi ambao umekuwa ukifanywa kwa makusudi kuwa Kinana anahusika na meli iliyohusika kusafirisha pembe zile.
“Uvumi huu ni uzushi, meli iliyobeba mizigo ile inaitwa Delmas Nakadha, mmiliki wake anaitwa Bus Herman Ledley jambo hili Kambi ya Upinzani Bungeni inalijua, ila kwa masilahi yasiyokubalika katika taifa wameamua kupotosha Bunge lako,” alisema.
Alisema baada ya uchunguzi wa kutosha, wahusika walibainika na ikafunguliwa kesi ya uhujumu uchumi namba 3 na 4 ya mwaka 2009 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
“Hawa (anawataja) ndiyo waliopelekwa kortini, uchunguzi ulijidhihirisha kuwa ndiyo watuhumiwa wa jambo hili, Kambi ya Upinzani Bungeni inalijua,” alisema.
CHANZO: mwananchi
0 maoni:
Chapisha Maoni