Mtwara. Wakati mtu mwingine akiripotiwa kufa,
hali bado ni tete katika Mji wa Mtwara kutokana na mabomu ya machozi na
risasi za moto kuendelea kurindima kwenye mitaa kadhaa wakati polisi
wakipambana na makundi ya vijana wanaopinga mradi wa ujenzi wa bomba la
gesi kwenda Dar es Salaam.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya
Ligula, Mohamedi Kodi alithibitisha kupokea mwili wa mjamzito ukiwa na
tundu tumboni, linaloaminika kuwa linatokana na risasi.
“Ni kweli kwa leo tumepokea maiti moja ya mwanamke
ambaye ni mjamzito wa miezi saba akiwa amepigwa risasi tumboni,”
alisema Dk Kodi. Inadaiwa kwamba mjamzito huyo ambaye jina lake
halikufahamika, ameuawa akiwa nyumbani kwake. Kifo hicho ni cha pili
baada ya Karim Shaibu (22), mkazi wa Chikongola kuuawa juzi.
Aidha, kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa
mtu mwingine ambaye jinsia yake haikujulikana aliuawa kwa bomu la
machozi na mwili wake kutawanyika barabarani.
Kuhusu majeruhi, Dk Kodi alisema wamefikia watu
18... “Majeruhi wa mwisho tuliyempokea ni mwanafunzi wa Shule ya
Sekondari ya Chuno. Alikuwa amevunjwa miguu yote kwa risasi.”
Waomba hifadhi hospitalini
Umati wa watu wengi wao wakiwa kinamama na watoto
umemiminika kwenye Hospitali ya Ligula kukimbia msako wa nyumba kwa
nyumba unaofanywa na polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati
tofauti, wakazi hao wamelalamikia kitendo cha polisi kuingia katika
makazi yao, kuwapiga na kuwapora mali zao.
“Magomeni A hatuna amani, askari wanaingia
nyumbani kwetu, wanatupiga na kutunyang’anya simu, yaani huku Magomeni
hatuna amani kabisa, tumepotezana na watoto na hatujui hata waume zetu
wako wapi,” alisema Paulina Idd.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara,
Linus Sinzumwa alisema hali ni shwari na kuwataka wananchi kuendelea na
shughuli zao kama kawaida.
Hadi sasa huduma za kijamii zimesimama, hakuna
maduka yaliyofunguliwa, hakuna usafiri wa daladala wala pikipiki, mji
upo kimya huku sauti za milio ya mabomu na bunduki ikitawala, wanajeshi
waliovalia sare wametapakaa sehemu mbalimbali za mji wakiwa katika
magari na pikipiki.
Nchimbi atua Mtwara, jeshi lamwaga vifaa
Dk Nchimbi aliwasili jana jioni kwa helikopta na
kukutana na viongozi wa Mkoa wa Mtwara walioongozwa na Mkuu wa Mkoa,
Kanali Joseph Simbakalia kujadili suala hilo.
Pia ndege kubwa ya jeshi nayo ilitua huko na wanajeshi walikuwa wakipakua vitu mbalimbali vilivyoaminika kuwa vifaa.
Jeshi hilo limeombwa kuongeza kukabiliana na vurugu hizo ambazo zimesambaa sehemu mbalimbali za Mtwara.
Imeandikwa na Haika Kimaro, Mary Sanyiwa na Elias Msuya.
0 maoni:
Chapisha Maoni