Dodoma. Shirika la Umeme nchini (Tanesco), limepata hasara ya
Jumla ya Sh966.18 milioni kutokana na wizi na uharibifu wa miundombinu
katika mikoa mbalimbali nchini, Bunge lililezwa jana.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato
na Matumizi kwa wizara hiyo kwa mwaka 2013/14.
Waziri huyo alisema, kiasi hicho ambacho ni sawa
na Dola za Marekani 603,862 kilipotea katika kipindi cha Julai 2012 hadi
Aprili 2013 ambapo ni hasara kubwa zaidi kwa Tanesco.
Kwa taarifa, ni wazi kuwa Tanesco imekuwa ikipata hasara ya karibu Sh96.7 milioni kila mwezi kiasi ambacho ni kikubwa.
“Wizi na uharibifu wa muda mrefu wa miundombinu ya
umeme kwa muda mrefu umekuwa ni tatizo sugu kutokana na wahusika kubuni
njia mbalimbali za kufanya uharibifu huo na kuisababishia Tanesco na
nchi kwa ujumla hasara kubwa,” alisema Muhongo.
Akizungumzia tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa
mara, alisema, “Tatizo la kukatika kwa umeme ni uchakavu wa miundombinu
ya usambazaji na vifaa vyake pamoja na kuzidiwa uwezo kwa mifumo yake.”
Kingine alitaja kuwa ni wizi wa nyaya za shaba na mafuta ya transfoma zaidi kwenye mikoa ya Arusha,Kilimanjaro na Mkoa wa Tanga.
Alitaja mkakati wa kukabiliana na tatizo hilo kuwa
ni pamoja na kubadilisha nguzo zilizoharibika katika njia za msongo wa
Kv 0.4 na Kv 11 na 33, kukata miti na kubadilisha vikombe vilivyovunjika
na nyaya chakavu.
Waziri alitaja miradi mingi ya umeme ambayo wizara
inajiandaa kuikamilisha katika maeneo mbalimbali nchini kuwa itagharimu
fedha nyingi.
Miradi hiyo ni ile ya MCC, REA ambayo inaendelea
kuzinduliwa katika maeneo tofauti na mingi imetekelezwa kwa kiwango cha
kuridhisha.
Kwa upande wao Kambi ya Upinzani waliitaka Wizara
ya Nishati na Madini kueleza ukweli kuhusu mgao wa umeme ambao
unaendelea kuwatesa Watanzania huku kukiwa na taarifa kuwa hakuna mgao.
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo, Msemaji wa
Upinzani katika Wizara ya Nishati na Madini,John Nchimbi aliituhumu
Serikali kuwa imekuwa ikikanusha kuhusu mgao huo wakati hali ni tofauti
na kauli ya Serikali.
0 maoni:
Chapisha Maoni