Jukwaa wa Wakristo Tanzania limemtaka Rais Jakaya Kikwete kutoa
msimamo wake kisheria ambao utaleta upatanisho kati ya waumini wa dini
ya Kiislamu na Kikristo.
Jukwaa hilo limesema kauli iliyotolewa na rais
juzi wakati wa sherehe za Mei Mosi, Mbeya ya kutaka Watanzania waishi
kama zamani ina utata kwa sababu imetafsiriwa tofauti na baadhi ya
Watanzania.
Hivi karibuni Rais Kikwete wakati akizungumza
kwenye sherehe za Mei Mosi alisema Serikali bado inaendelea kuzungumza
na viongozi wa dini wa pande zote na kuwaunganisha ili kuona maelewano
yanarejea kama ilivyokuwa zamani na kuwataka Watanzania waendelee kuishi
bila kubaguana au kuchukiana kwa dini zao.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa jukwaa hilo,
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu
wa Kikatoli Tanzania (TEC), alisema licha ya maneno hayo kuwa mazuri
lakini bado kuna utata kwa sababu baadhi ya raia wameingiwa na wasiwasi.
Alisema maeneo mengine wakristo hawali nyama kwa
sababu hawataki kulazimishwa kula nyama zilizochinjwa kwa ibada za
kiislamu na kwamba suala hilo siyo dogo kama wengine wanavyofikiri kwa
sababu limegharimu maisha ya watu.
Alisema licha ya kuwapo kwa kauli za uchochezi wa
kuwaua viongozi wa dini ya kikristo,kuchoma makanisa na mauaji ya
viongozi wa kikristo bado hazijafutwa wala waliozitoa hawajakamatwa na
kwamba hawajui kinachoendelea.
Mwenyekiti huyo alisema madai ya msingi ya
waislamu yaliyosababisha waanzishe vurugu na mauaji hayajajibiwa na
Serikali huku maswali yaliyoulizwa na wakristo kutokana na madai hayo na
vurugu hizo nayo yakiwa hajayajibiwa.
Alisema licha ya kukutana na Rais Kikwete Aprili
23, mwaka huu ambaye alihimiza viongozi wa wakristo na waislamu wakutane
ili kuondoa tofauti zao zisizo za kiimani lakini bado wanasubiri
maelekezo toka serikalini kwani ajenda ya uvunjifu wa amani viongozi wa
dini hawawezi kuizungumzia kwa sasa bila majibu ya Serikali kwa madai
yaliyozua uvunjifu huo wa amani.
0 maoni:
Chapisha Maoni