Dar es Salaam. Tukio la kutupwa bomu katika Kanisa Katoliki la
Joseph Mfanyakazi, Arusha limetua katika Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa (UN) baada ya kuwasilishwa na Balozi wa Vatican UN, Askofu Mkuu
Frances Chullikatt.
Askofu Chullikatt anakuwa kiongozi wa kwanza wa
Vatican kutoa tamko kuhusiana na shambulizi hilo ambalo mmoja wa
viongozi wake alikuwapo.
Bomu hilo lilirushwa katika kanisa hilo wakati
likizinduliwa na Balozi wa Vatican nchini, Askofu
Mkuu Francisco Padilla Mei 5, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi zaidi ya 50.
Mkuu Francisco Padilla Mei 5, mwaka huu na kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi zaidi ya 50.
Wakati wa shambulizi hilo, Askofu Padilla na Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, Josephat Lebulu walionusurika.
Akihutubia Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa, New York, Marekani juzi, Askofu Chullikatt alisema tukio
lililotokea Arusha linadhihirisha kuwa kuna umuhimu ya kupambana na
ugaidi katika Afrika ili kuimarisha amani na usalama wa kimataifa.
“Unahitajika mshikamano na ushirikiano wa pamoja
wa mataifa mbalimbali katika kuchukua hatua za maisha na kulinda haki za
binadamu,” alisema Askofu Chullikatt, ambaye amekuwa mwakilishi wa
Vatican kwenye Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2010.
Askofu Chullikatt, ambaye ni mzaliwa wa India,
alisema suala la ugaidi linahitaji kuzuiwa duniani kote na hasa Afrika
kutokana na matukio hayo kuharibu maisha ya binadamu na kutokea katika
maeneo wanayofanyia ibada.
Askofu Chullikatt alisema pale ugaidi unapofanyika
kwa kutumia dini, waumini na viongozi wao ni lazima wahakikishe
wanapambana nao ili kuutokomeza.
Alisema suala la ugaidi linahitaji viongozi wa
kisiasa, kijamii na kidini kulilaani kwani ni la kikatili katika maisha
ya binadamu hivyo si vyema kukaa kimya suala hilo linapotokea.
Askofu Chullikatt alisema ugaidi unaotokea Afrika
unatakiwa kuangaliwa kimataifa ili kuzipa uwezo nchi hizo kupambana na
kuzuia matukio hayo.
Shambulio la bomu dhidi ya kanisa la Arusha lilikuwa tukio la pili la ugaidi uliolenga kushambulia wageni nchini.
Mara ya kwanza ilitokea mwaka 1998, wakati Ubalozi
wa Marekani nchini ulipolipuliwa kwa bomu na kusababisha vifo vya watu
kumi na moja huku 85 wakijeruhiwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni