Dar es Salaam. Bandari ya Dar es Salaam imekuwa
ikilikosesha taifa Dola 1.8 bilioni za Marekani (Sh2.8 trilioni) kwa
mwaka, kutokana na kukosa ubora wa biashara.
Kutokana na hali hiyo, wataalamu wameeleza kuwa
bandari hiyo inahitaji kufanyiwa maboresho muhimu ya hali ya juu, ili
fedha hizo zisaidie nchi kuacha kutegemea misaada ya maendeleo.
Kwa mujibu wa ripoti iliyopo kwenye kitabu cha
Opening the Gates: How the port of Dar es Salaam can transform Tanzania,
licha ya Bandari ya Dar es Salaam kuwa sehemu nzuri, imekosa uwezo
hivyo usimamiaji sera bora za kuiboresha zinatekelezwa taratibu. Ripoti
hiyo inaeleza kuwa, mwaka 2012 pekee bandari hiyo ilikosesha taifa kiasi
hicho cha fedha, huku ikizikosesha nchi jirani Sh1.3 trilioni.
“Fedha hizo ni sawa na asilimia saba ya pato la
taifa, kitu ambacho kinawaathiri wanunuzi, wafanyabiashara na wakala
mbalimbali wa Serikali,” inaeleza.
Mchumi Mkuu wa Benki ya Dunia (WB), Jacques
Morisset ameihimiza Tanzania kuifanya bandari hiyo kuwa moja ya
vipaumbele vyake vya juu kwa ajili ya kukua kwa uchumi.
“Watumiaji Bandari ya Dar es Salaam wanalipa fedha
nyingi kwa wasimamizi wa bandari na wakala mbalimbali, kwa ajili ya
huduma zao kuliko Mombasa,” alisema Morisset.
Akizungumzia ripoti hiyo, Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe alisema Serikali imekuwa ikijitahidi kuboresha
bandari hiyo, lakini kazi ya ziada inahitajika kuifanya iweze kushindana
na nyingine. “Tunahitaji nchi jirani ziendelee kuitumia bandari yetu,
bado tuna kazi kubwa ya kufanya ndiyo maana niko hapa, tunahitaji
kuimarisha Kitengo cha Operesheni na maeneo mengine,” alisema Dk
Mwakyembe.
0 maoni:
Chapisha Maoni