Sumbawanga. Polisi katika Mkoa wa Rukwa likishirikiana na Polisi
wa Tabora pamoja na kikosi kazi maalumu cha kitaifa, limefanikiwa
kuwatia nguvuni watu tisa waliokuwa wakisakwa kwa muda mrefu kwa tuhuma
za kumkata mkono, Mwigulu Matonange(10) mlemavu wa ngozi Februari 15
mwaka huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwarwanda
alisema watuhumiwa hao walikuwa wakisakwa kwa muda mrefu kutokana na
mtandao mkubwa waliokuwa nao, hatimaye baadhi wamefanikiwa kukamatwa
huku wengine bado wakiendelea kutafutwa.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Weda
Mashilimu(29),Nickon Kadogoo(25), Peter Msabato(32),Ignas
Sungura(27),Faraja Mwezimpya (31) pamoja na Kurwa Hamis (29) wote wakiwa
ni wakazi wa Kijiji ha Ilemba Rukwa.
Aliwataja watuhumiwa wengine ambao ni Hamis
Mnywanywa ambaye ni mganga wa jadi na mkazi wa Karema Katavi,James
Paskali(24) mkazi wa majimoto, pamoja na Ibrahimu Tella(27) mkazi wa
kijiji Masanula-Usule Shinyanga.
Kamanda alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao
kulifuatia uchunguzi wa kina uliokua unafanywa na polisi hao kupitia
mawasiliano ya simu na taarifa mbalimbali za kipelelezi ambapo siku ya
April 22 walifanikiwa kumnasa Nickon Kadogoo akiwa Katavi na mkono huo
akiupeleka mkoani Tabora ambapo angepata soko.
Baada ya kuhojiwa mtuhumiwa huyo alidai kuwa yeye
na wenzake hao waliagizwa mkono huo na mganga wa jadi aitwaye Rashid
Manywanywa, ambapo aliwaahidi angemlipa kila mmoja Sh600 milioni kama
wangempelekea mkono huo.
Alisema baada ya tukio la kumkata mtoto huyo mkono
na kumpelekea mganga huyo alidai kuwa hana fedha zote hizo kwani wao
walishindwa kutumia akili kwa kuwa hata yeye ni maskini angelipata wapi
fedha zote hizo, hivyo hawezi kununua mkono huo.
Baada ya kuona soko limeshindikana ndipo
walipoamua kufanya mawasiliano na watu wengine na kuhakikishiwa katika
Mikoa ya Tabora na Shinyanga kuna soko la uhakika ndipo safari ya
kuelekea huko ikaanza.
Kwa upande wake, mganga huyo wa jadi alikiri
kuwaagiza watuhumiwa hao mkono huo na kudai kuwa alitaka kutumia
kutengenezea chombo cha usafiri ambacho alidai kuwa ni ungo ambao
unatumika na wachawi kusafiria nyakati za usiku.
Kamanda huyo alisema watuhumiwa wote kutoka mikoa
hiyo wamekamatwa na polisi na bado upelelezi unaendelea mara baada ya
kukamilika watafikishwa mahakamani wakati wowote.
0 maoni:
Chapisha Maoni