Dar es Salaam. Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi na aliyekuwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) sasa Umoja wa Afrika
(AU), Dk Salim Ahmed Salim wamekuwa kwenye mkakati mkali wa kulinusuru
Jengo la Makao Makuu ya Chama cha Skauti Tanzania lisiuzwe.
Hatua hiyo inatokana na baada ya Mahakama Kuu
Kitengo cha Kazi kuamuru jengo hilo liuzwe ili kufidia deni la zaidi ya
Sh111 milioni ambalo kilikuwa kinadaiwa chama hicho. Hati ya kukamatwa
jengo hilo namba 1078 lililopo kiwanja namba LO 120652 ilitolewa Aprili
24, mwaka huu kupitia Kampuni ya Udalali ya Flamingo Auction Mart ambayo
imetoa muda wa siku 14 fedha hiyo ilipwe au nyumba hiyo ipigwe mnada.
Gazeti hili lilitembelea ofisi za chama hicho jana
na kukuta hati ya kukamatwa jengo hilo iliyosainiwa na Dalali wa
Mahakama Deogratius Luziga ikiwa imebandikwa ukutani. Kwa mujibu wa hati
hiyo fedha inayodaiwa ni Sh111,510,384 kupitia shauri namba 175/2009
ambapo mdai ni Agnes George aliyekuwa mfanyakazi wa chama hicho.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ya
chama hicho, Brigedia Jenerali Mstaafu Gerald Mkude alisema wanategemea
katika kipindi cha siku 14 watashughulikia suala hilo ili kulinusuru
jengo hilo lisiuzwe.
“Tulikutana na wadhamini wa chama (Mwinyi na Dk
Salim) juzi na baada ya kujadiliana walitoa mapendekezo na maagizo ya
kuchukua ili kuokoa jengo hilo,” alisema Mkude.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo hakuwa tayari kueleza
mapendekezo hayo na kudai hawajafikia mwisho wa utekelezaji wa maagizo
si rahisi kuyatamka kwa sasa.
Alisema mdai alikuwa katibu muhuktasi wa chama
hicho na kwamba alilazimishwa kuacha kazi mwaka 2007 baada ya kutokea
matatizo ya kiofisi.
Alisema wakati anaacha kazi madai yake yote
yalikuwa ni Sh3.6 milioni lakini kutokana na sababu za kiutawala
alilipwa mshahara wa mwezi mmoja tu.
Alisema hatua hiyo ilisababisha mfanyakazi huyo
kuwasilisha madai yake katika Mahakama ya Kazi mwaka 2009 ambapo
iliamriwa gari la chama hicho liuzwe.
0 maoni:
Chapisha Maoni