Tumezoea kila inapofika tarehe moja ya mwezi Mei kusherehekea siku ya
wafanyakazi duniani. Siku hii hutumiwa na viongozi wa vyama vya
wafanyakazi nchini hasa kudai masilahi kwa Serikali.
Tunakumbuka
mwaka 2010 ambapo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta)
liliandaa mgomo wa wafanyakazi likidai nyongeza za mishahara,
marekebisho ya pensheni na kodi kwenye mishahara.
Mgomo ule
uliiitikisa mno Serikali, kwani hata kwenye Mei Mosi ya mwaka ule,
mwajiri mkuu Rais Jakaya Kikwete hakualikwa. Wafanyakazi walibaki peke
yao na kujadili kero zao. Japo baadaye Rais Kikwete aliuzima mgomo huo,
bado madai ya wafanyakazi yameendelea kupigwa kalenda.
Hata hivyo,
katika Mei Mosi ya mwaka huu iliyofanyika jijini Mbeya juzi, Rais
Kikwete ameahidi neema kwa wafanyakazi ikiwa ni pamoja na nyongeza ya
mishahara na punguzo la kodi katika mishahara hiyo.
Hata hivyo,
ukweli unabaki kuwa bado kuna deni kubwa kwa Watanzania walio wengi. Kwa
muda mrefu Serikali imekuwa ikishughulikia tu kero za watu wenye ajira
ambao kimsingi ni wachache, japo hata kero zenyewe hazitatuliwi
kikamilifu. Ukiangalia idadi ya wafanyakazi waliopo katika utumishi wa
umma na wale wa sekta binafsi haizidi milioni moja kati ya Watanzania
zaidi ya 44 milioni.
Hao ndiyo Serikali inayowatangazia neema huku
kukiwa na kundi kubwa la wasio na ajira. Kati ya Watanzania milioni 44,
asilimia 82 ya wenye umri wa kuajiriwa wanajishughulisha na kilimo tena
cha kujikimu.
Kila mwaka kuna vijana zaidi ya 800,000 wanaomaliza
shule za msingi, sekondari na vyuo wanaingia kwenye soko la ajira.
Hivyo, kila mwaka kuna ongezeko la watu wasio na ajira hali inayotishia
amani huko tuendako. Kwa bahati mbaya kundi hili la wasio na ajira
halina mtetezi, hali chama kama vilivyo vyama vya wafanyakazi wala
halina msemaji, kila mtu anakufa kivyake.
Kuna wakati ulizuka mjadala
wa tatizo la ajira kwa vijana ambapo Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward
Lowassa alionya kuwa vijana wasio na ajira ni bomu litakalolipuka siku
za usoni. Lakini kwa harakaharaka, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka aliibuka na kumjibu Lowassa akitaka orodha ya mikakati ya
Serikali kwa kundi hilo. Hata hivyo, bado mikakati mingi iliyotajwa na
Kabaka siyo endelevu.
Kwa mfano, muundo wa Serikali yetu haulengi
kutatua tatizo la ajira kwa vijana. Mambo ya vijana yamewekwa katika
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na michezo. Kama kweli Serikali
inalenga kuwasaidia vijana katika suala la ajira, kwa nini isiwachukue
kwenye Wizara ya Kazi na Ajira?
Ninachokisema hapa ni Serikali kuweka mazingira bora kwa watu wasio na ajira ili wazipate. Ziwe rasmi au zisizo rasmi.
Kwa
mfano, idadi hii kubwa ya Watanzania wanaojishughulisha na kilimo nayo
itazamwe. Ni lazima kilimo hiki kirasimishwe, wakulima na wafugaji wawe
na uhakika wa kupata ardhi ya kilimo na malisho. Wapate pembejeo na
masoko kwa wakati.
Ukishatatua kero ya ajira kwa asilimia 82 ya wananchi, hapo angalau unaweza kupumua.
Kwa
upande wa wafanyakazi nao, Mei Mosi isiwe siku ya kulilia nyongeza za
mishahara, kupunguzwa kwa kodi na masuala ya pensheni peke yake. Wala
siyo siku ya kumwalika Rais na kuselebuka naye jukwaani tu.
Hii
inapaswa kuwa siku ya kujadili mustakabali wa kazi na maisha yetu. Kama
kazi ni kipimo cha utu, uko wapi huo utu ikiwa asilimia zaidi ya 80 ya
Watanzania hawana ajira za uhakika? Tukumbuke kuwa idadi hiyo ni mzigo
kwa walio na ajira rasmi.
0 maoni:
Chapisha Maoni