Jumatatu, 29 Aprili 2013

Nyumba nyingi kuporomoka nchini

Dar es Salaam. Imebainika kuwa nyumba nyingi zilizopo jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, zipo hatarini kubomoka kutokana na kujengwa kwa matofali yasiyokuwa na ubora.
Pia, hatua hiyo inatokana na kutokuwapo kwa ukaguzi wa vifaa mbalimbali vya ujenzi yakiwamo matofali ya saruji yanayotumika katika ujenzi wa nyumba hizo.
Uchunguzi uliyofanywa na Mwananchi hivi karibuni jijini Dar es Salaam na baadhi ya maeneo nchini, umebaini kuwepo kwa ongezeko kubwa la biashara holela ya matofali yanayotengezwa kwa ubora hafifu.
Uchunguzi pia unaonyesha kutokuwapo kwa usimamizi wa kutosha katika sekta ya ujenzi nchini ni moja ya vyanzo vya watu kufanya biashara ya vifaa vya ujenzi kiholela.
Biashara hizo ni pamoja na uuzaji wa matofali yasiyokuwa na viwango kutokana na kukosa udhibiti maalumu.
Moja ya mambo yanayosababisha matofali yanayotumika katika ujenzi jijini Dar es Salaam kuonekana kuwa hayana ubora ni utengenezaji wa matofali hayo.
Imegundulika kuwa saruji inayotumika katika utengenezaji huo ni ndogo na mchanga unakuwa mwingi kwa lengo la kutengeneza matofali mengi ili kupata faida.
Wakati uchunguzi huo ukionyesha hivyo Mwananchi, ilimtafuta Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Mhandisi Boniface Muhegi, ambaye alishauri kufanyika kwa uchunguzi wa bidhaa zinazotumika katika ujenzi.
Muhegi anasema “Ili kuepusha madhara hasa kuanguka kwa majengo ni vyema Shirika la Viwango Tanzania (TBS), likachukua hatua ya kufanya ukaguzi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi ili kuongeza usalama katika masuala ya ujenzi.|
Anasema ili kuhakikisha kuwa majengo yanakuwa salama, ni vyema watu wakatumia wakandarasi waliosajiliwa ili kuwabana wakati kunapotokea madhara.
“Sisi tunashauri kwamba kama mtu anataka kujenga nyumba amayo ni salama, ni vyema akatumia wakandarasi waliosajiliwa ili iwe rahisi kuwabana wakati tatizo lolote linapojitokeza,”anasema.
Mhandisi Muhegi anasema “Ni vyema wananchi nao wakatambua kwamba matumizi ya vifaa visivyokuwa na viwango sio salama kwa maisha yao”.
Anasema kila mmoja aone haja ya kutumia vifaa vyenye ubora ili kujihakikishia usalama wa makazi yake na kuepusha kutokea kwa majanga mbalimbali.
“Kama tutakuwa makini katika matumizi ya vifaa bora vya ujenzi tutakuwa na makazi salama na tutaepusha majanga mbalimbali.
NUKUU
Machi 29 mwaka huu jengo la ghorofa 16 liliporomoka jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 30.
Febuari 17 mwaka huu, jengo lingine la ghorofa tatu liliporomoka huko Sinza Mori Dar es Salaam na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wawili waliokolewa na vikosi vya uokoaji.
Mwaka 2006 Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliunda tume ya kufuatilia ujenzi wa maghorofa na kubaini kuwa zaidi ya majengo 100 jijini Dar es Salaam yamejengwa bila kuzingatia vigezo.
Msomaji wetu kama una maswali yoyote kuhusiana na ujenzi na ubora wa majengo unaweza kumuuliza Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), kwa kutuma kupitia baruapepe: mwananchijumamosi@yahoo.com au ujumbe wa simu kupitia namba: 0658 376410

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More