WABUNGE katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao walihudhuria mafunzo ya kijeshi
katika kambi tofauti za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), walipata msoto wa
nguvu.
Kuonesha jinsi ambavyo msoto ulikuwa wa nguvu, katika kambi ya Tanga, siku tu ya utambulisho, mbunge wa Chadema (jina tunalo), alizimia.
Vilevile, kwenye Kambi namba 832, Ruvu, Pwani, Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine, alishindwa kuhimili kishindo cha depo, hivyo akatoroka, japo mafunzo yenyewe yalikuwa ya muda wa wiki tatu tu.
Baadhi ya wabunge wakiwa katika pozi na wanajeshi wengine.
ILIKUWA KAZI KWELI
Siku ya kwanza tu ya kuripoti kambini, wabunge wote walipigwa vipara na baada ya hapo, ilifuata awamu ya kupima afya.
“Jeshi ni jeshi tu, tulipimwa ukimwi bila hata kuandaliwa wala kupewa ushauri,” alisema mmoja wa wabunge waliohudhuria depo hiyo (jina tunalo) kisha akaongeza: “Mfano mimi ningeambiwa kule kuna kupima ukimwi hata nisingeenda, nilikuwa sijapima kama miaka saba, dah kule ni hatari.”
KUHUSU VIPARA
Mbunge mwingine alisema: “Walichotuweza ni ile tunaripoti tu, tunanyolewa vipara halafu ndiyo taratibu nyingine zinafuata. Kama wangekuwa wanatuonesha picha ya kile kitakachofanyika kabla ya kutunyoa, wengi wetu tungetimka mapema.
“Tatizo unanyolewa halafu ndiyo unapelekwa kupimwa ukimwi, sasa ukikataa kupima na una kipara chako, mtaani utarudi vipi? Hata kunyoa, wengine tuliingia na rasta, lakini wakatupiga upara wa wembe harakaharaka bila hata kungoja kuzifumua.”
MAFUNZO YANA FAIDA?
Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Umoja wa Vijana wa CCM, Mkoa wa Mara, Ester Bulaya, alisema kuwa anashukuru kupata mafunzo ya kijeshi, kwani yamemjenga kwa kiasi kikubwa.
“Japo ni kazi lakini tunatamani muda uongezwe, maana wiki tatu zilikuwa fupi, program ni nyingi, kwa hiyo tukatakiwa kufanya kwa pamoja,” alisema Bulaya kisha akaongeza: “Imenijenga kweli, najiona mkakamavu mwenye uwezo zaidi wa kutumikia wananchi.”
Kwa upande wa Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, alisema: “Natamani kila mtu awe anapitia mafunzo ya JKT, maana siyo tu yanakujenga kiukakamavu, bali pia yanakupa uzalendo na ari ya kuwatumikia wananchi.”
0 maoni:
Chapisha Maoni