Jumamosi, 27 Aprili 2013

CHAMA CHA CUF CHAHUSISHWA NA FUJO ZA LIWALE

 
MBUNGE wa Liwale, Faith Mitambo (CCM), amekishutumu Chama Cha Wananchi (CUF) kwamba ndicho kilichoasisi vurugu zilizotokea jimboni kwake. Mbunge huyo pia alilaumu Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka kudhibiti machafuko hayo na badala yake kuwaacha wafuasi wa chama hicho kufanya uharibifu wa mali za watu.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, katika vurugu hizo amepoteza nyumba zake mbili zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 100, huku wengine wakichomewa magari na maduka.

Akizungumza na MTANZANIA juzi kwa njia ya simu, Mitambo alisema vurugu hizo hazitokani na suala la stakabadhi ghalani pekee bali pia kuna siasa chafu ambazo zimeingizwa.

“Tatizo hili si la stakabadhi ghalani peke yake, CUF wamekuwa wakifanya mipango hii siku nyingi na ilikuwa wafanye maandamano April 15, mwaka huu.

“Lakini yalizuiliwa, leo hii yametokea yaliyotokea, lakini ni vyema wakafahamu kuwa ni complete unfair kwani kuchoma na kutuharibia mali zetu ni kutuonea.

“Ukiangalia mali zote zilizoharibiwa ni za viongozi wa CCM, mimi ni mbunge wa CCM, mwenyekiti wa CCM nyumba yake imechomwa na madiwani wa CCM.

“Viongozi mbalimbali wa CCM nyumba zao zimeharibiwa vibaya kwa moto, huu ni uonevu mkubwa ndiyo maana nasema tatizo sio korosho kuna siasa chafu ndani yake,” alisema Mitambo.

“Nilipopata taarifa hizo asubuhi juzi niliwasiliana na vyombo vya dola, RPC na OCD niliwapa taarifa mapema lakini hawakutoa msaada wowote hadi nyumba zetu zikateketezwa.

“Mimi nimesikitika kama vyombo vya dola unaweza kuwasiliana navyo vikashindwa kutoa msaada hadi kusababisha mali kuharibika ni tatizo kubwa,” alisema.

Alisema tatizo la stakabadhi ghalani wamekuwa wakilipigia kelele kila siku na wamekuwa wakikutana kwa lengo la kulipatia suluhu.

“Ni miezi saba sasa, kipindi chote tumepiga kelele kuomba Serikali ilifanyie kazi, wiki mbili zilizopita ndiyo wamenza kuuza korosho na kulipwa,” alisema.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More