“Mimi kama Waziri wa Uchukuzi sina tatizo na ongezeko hili dogo la nauli za daladala. Tatizo langu ni tabia yetu ya Watanzania wengi kukacha vikao halali vinavyojadili mambo yanayotuhusu na kuja kulalamika baadaye,” alisema Dk Mwakyembe.
Dk Mwakyembe alisema upandishwaji huo ulifuata vigezo vyote hivyo hakuna sababu za kulalamika. Alisema kiwango kilichopandishwa ni kidogo ukilinganisha na jinsi wamiliki wa vyombo husika walivyokuwa wameomba.
Alizitaja hatua zilizopitiwa kuwa ni pamoja Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), kuitisha mikutano ya wazi na wadau kwa ajili ya kupokea maoni yao.
Hata hivyo, aliwaonya wamiliki wa vyombo hivyo watakaokiuka na kupandisha nauli kwa kiwango cha juu akisema lazima ‘atakula nao sahani moja’.
Alisema wawakilishi wote wa abiria waliambiwa kama ongezeko hilo dogo la Sh100 hawaridhiki nalo, sheria inawaruhusu kukata rufani katika Baraza la Ushindani na kwamba hakuna aliyefanya hivyo na kubaki kulalama nje ya taratibu.
“Mimi kama Waziri wa Uchukuzi sina tatizo na ongezeko hili dogo la nauli za daladala. Tatizo langu ni tabia yetu ya Watanzania wengi kukacha vikao halali vinavyojadili mambo yanayotuhusu na kuja kulalamika baadaye,” alisema Dk Mwakyembe.
Alisema awali watoa huduma ya daladala waliomba kupandisha nauli kutoka Sh300 hadi Sh872 kwa abiria sawa na ongezeko la asilimia 149.
Alisema baada ya majadiliano hayo, Sumatra ilikubali nauli hiyo iongezwe kwa Sh100 tu kwa watu wazima na Sh50 kwa wanafunzi ili kugawana maumivu ya gharama za uendeshaji kwa watoa huduma.
Dk Mwakyembe alisema ni kweli gharama za uendeshaji kwa wenye mabasi zimeongezeka ikiwamo bei za mafuta pamoja na vifaa mbalimbali kama matairi.
Waziri huyo pia aliunga mkono ongezeko la nauli katika usafiri wa reli na mabasi yaendayo mikoani kuwa nauli zao hazijapandishwa kwa kiwango kikubwa hivyo haoni ni kwa nini Serikali isikubali.
0 maoni:
Chapisha Maoni