Dar es Salaam. Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema
ameibuka kidedea baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi ya
marejeo ya rufaa iliyomrejesha bungeni.
Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo na
makada watatu wa CCM mkoani Arusha, kupitia kwa Mawakili wao Alute
Mughway na Modest Akida wakiiomba Mahakama ya Rufani ifanye marejeo ya
hukumu yake hiyo kwa madai kuwa hukumu hiyo haikuwa sahihi.
Hata hivyo, jana Mahakama ya Rufani ilisikiliza
maombi hayo kutoka kwa waombaji pamoja na hoja za wajibu maombi na kisha
kutupilia mbali maombi hayo ikisema kuwa hayana msingi.
Uamuzi huo wa kutupilia mbali maombi hayo ulisomwa
na Jaji Bernard Luanda, kwa niaba ya jopo la majaji wenzake lililokuwa
likiongozwa na Engela Kileo na Salum Massati.
Hata hivyo, jopo hilo halikutoa sababu za kutupilia mbali maombi hayo na badala yake lilisema litatoa maelezo ya kina baadaye.
Majaji hao isipokuwa Kileo ndiyo waliosikiliza na
kutoa hukumu ya rufaa iliyomrejesha Lema bungeni, ambayo ilikuwa
inapingwa na makada hao wa CCM.
Awali, kabla ya kutupilia maombi hayo ya marejeo,
mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya waombaji hao kutaka suala hilo
lisikilizwe na jopo la majaji saba.
Wakili Mughwai aliwasilisha maombi katika Mahakama
ya Rufani akiomba marejeo ya rufaa yahamishwe katika jopo la majaji
watatu na kupelekwa kusikilizwa na jopo la majaji saba kwa madai kuwa
kuna jambo linatakiwa kushughulikiwa kutokana na mazingira yake.
Wakili wa Lema, Methods Kimomogoro alidai kuwa
Wakili Mughwai amechanganya maombi hivyo kuleta utata na kwamba kama
alikuwa akitaka yasikilizwe angeyapeleka katika utaratibu ulio sahihi.
“Kanuni ya Nne ya Mahakama ya Rufaa, inasema
hakuna kanuni rasmi inayowezesha jopo hili kuhamisha maombi ya marejeo
kwenda kwenye jopo la majaji saba kwa ajili ya mapitio,” alisema
Kimomogoro na kuongeza:“Labda kama maombi ya mapitio yangekubaliwa,
wangekwenda hatua ya pili ya kuomba jopo la majaji saba.
Maombi haya hayajafuata utaratibu hivyo naomba
Mahakama iyatupilie mbali kwa kuwa sababu za kisheria hazikidhi na
Mahakama haina uwezo wa kuyatolea uamuzi.”
Wakili wa Serikali, Vicent Tangoh alimuunga mkono
Kimomogoro na kuongeza kuwa hiyo inaonyesha hakuna maombi yoyote mbele
ya Mahakama wala kitu cha kupeleka katika jopo la majaji saba.
Kutokana na hoja hizo, Jaji Luanda kwa niaba ya jopo
alikubaliana na hoja za wajibu maombi na hivyo akayatupilia mbali maombi
hayo.
Lema alivuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu Kanda
ya Arusha, Aprili 5, 2012 baada ya kesi iliyofunguliwa na wanachama
watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga
ushindi wake katika uchaguzi mkuu mwaka 2010.
0 maoni:
Chapisha Maoni