Jumamosi, 13 Aprili 2013

Lwakatare aligawa Bunge

SAKATA la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Rwezaula kushtakiwa kwa makosa ya ugaidi, limeibua mvutano mkali bungeni huku wabunge wakishambuliana kwa maneno makali.
Mvutano huo uliibuka jana wakati wa kujadili hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ambapo Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) alichafua hewa wakati akichangia na kudai kuwa aliyerekodi video ya Lwakatare yupo tayari kuja kutoa ushahidi.
Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara) aliliambia Bunge kuwa CHADEMA wasihangaike kujitetea kwa swala la Lwakatare kwani ushahidi wote kuhusu video hiyo upo na kwamba yuko tayari kuutoa bungeni, duniani na mbinguni.
“Nataka nitoe ufafanuzi kuhusu suala la ugaidi ambalo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amezungumza kwenye hotuba yake hapa bungeni jana. Aliyerekodi mkanda yupo na mimi niko tayari kuhojiwa popote hata mbinguni,” alisema Mwigulu na kuibua nderemo kutoka kwa wabunge wa CCM.
Mwigulu alionyesha karatasi aliyodai kuwa ilitumiwa na Lwakatare kupanga kile alichodai kuwa ni mkakati wa mauaji akisema huo ndiyo mkakati wa CHADEMA kupanga mauaji na kwamba viongozi wakuu wa chama hicho wanapaswa kushtakiwa.
Bila kujali kwamba suala hilo liko mahakamani wala ni kinyume cha kanuni za Bunge kumtaja mbunge mwingine kwa jina akimtuhumu, Mwigulu alisema anaishangaa CHADEMA kumtaka yeye aunganishwe kwenye kesi kwa kuwa na mawasiliano na mmoja wa watuhumiwa wakati hata wao wana mawasiliano na Lwakatare.
“Alisema Mbowe hapa jana kuwa mimi napaswa kushtakiwa kwa ugaidi, ingawa simuoni hapa ndani labda tayari amekwishakamatwa na polisi, lakini nataka kusema kuwa watu hawa ni waongo na wanafiki. Wanapanga mauaji halafu wanakuja hapa kuwahadaa wananchi kuwa wanapinga ugaidi,” alidai.
Hatua hiyo ya Mwigulu kumtaja Mbowe kwa jina na chama chake kuwa ni magaidi, iliwashtua baadhi ya wabunge wakishangaa kuona Spika wa Bunge, Anne Makinda akishindwa kutumia kanuni kumbana na kumtaka afute kauli ana atoe uthibitisho.
Baada ya kuona Makinda anakuwa na kigugumizi, baadhi ya wabunge wa CHADEMA, Joseph Selasini (Rombo), Mustafa Akunaay (Mbulu), Pauline Gekul (Viti Maalumu) walijaribu kusimama kuomba mwongozo lakini walikataliwa.
Hata hivyo, Akunaay aliendelea kuomba mwongozo akitaka Mwigulu aache kuzungumzia suala hilo kwa vile liko mahakamani, lakini Spika Makinda alisimama na kusema kwamba kama ni suala la kanuni zifuatwe kwa wote.
Spika Makinda ambaye alionekana kukitetea chama chake cha CCM alitumia mafumbo kuwajibu wabunge wa CHADEMA akiwataka kuacha tabia ya mkuki kwa nguruwe kwa binadamu mchungu.
“Jana Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe alizungumzia suala la ugaidi na kesi iliyopo mahakamani, hakuzuiliwa. Leo mnamzuia Mwigulu. Kama ni kanuni ziwe kwa wote si mkuki kwa nguruwe halafu kwa wengine...,” alisema. 
Baada ya Mwigulu kuchangia ndipo Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) alipata nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu na kuzungumzia maeneo matatu ya elimu, usalama wa nchi na katiba mpya.
Katika suala la usalama, Lissu alijielekeza moja kwa moja kupangua makombora ya Mwigulu bila kumtaja kwa jina, akisema Jeshi la Polisi limekuwa na mawasiliano na baadhi ya watu ndani ya Bunge kufanya vitendo vya kigaidi na kuwapakazia watu wengine.
“Kwa muda mrefu Jeshi la Polisi limekuwa likituhumiwa kufanya vitendo vya uhalifu na kushirikiana na watu humu ndani kupanga vitendo vya kigaidi na kuwasingizia watu wasio na hatia. Hii haikubaliki,” alisema Lissu.
Lissu alisema kuwa mmoja wa watuhumiwa wa ugaidi wanaoendelea kushikiliwa mahabusu amekuwa akifanya mawasiliano ya simu na mmoja kati ya wabunge kupanga njama za ugaidi na kuwabambikia watu wasio na hatia.
Alienda mbali kwa kusema kuwa kiongozi huyo ambaye yumo ndani ya Bunge, alituma pesa kwa njia ya simu kwa mmoja wa watuhumiwa hao wa ugaidi kwa ajili ya kupanga ugaidi.
Wakati akiendelea na hotuba yake, Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah (CCM) aliomba mwongozo wa Spika kuhoji kama Lissu ana ushahidi wa mambo anayosema.
Alipotakiwa na Spika kujibu swali hilo, Lissu alisema mawasiliano ya kwanza kati ya kiongozi huyo na mtuhumiwa mmoja wa ugaidi, yalifanyika Januari 24 mwaka jana.
“Mawasiliano ya pili yalifanyika Desemba mwaka jana ambapo kiongozi huyo alituma pesa kwa mtuhumiwa huyo. Mheshimiwa Spika tuna ushahidi wa kutosha kuhusu hilo,” alisema Lissu.
Hata hivyo, hatua ya Spika kukatiza hotuba ya Lissu na kumpatia nafasi Abdallah kuomba mwongozo ililalamikiwa na wabunge wa upinzani ambapo wengine walikuwa wakizomea na kudai kuwa anapendelea.
Lissu aliendelea na mchango wake akisema “sheria ya ugaidi inasema anayetoa fedha kufadhili ugaidi naye ni gaidi, akamatwe, afungwe.”
Mbali ya kuzungumzia suala hilo la ugaidi, Lissu alisisitiza kauli ya Mbowe juzi kuwa CHADEMA haitashiriki kwenye mchakato wa katiba kama kasoro zilizoainishwa hazitarekebishwa.
Alisema CHADEMA ikijitoa haitabaki kimya, bali itazunguka nchi nzima kuwataka wananchi kutoipigia kura ya ndiyo.
Lissu alisema Kenya na Zimbabwe zilishamwaga damu kutokana na katiba na kuitahadharisha serikali kuwa makini na mchakato huo.
Pia alijadili suala la elimu akisema kuwa sasa ni wakati wa kuwajibishana na sio kutafuta mchawi.
“Waziri Mkuu amesema kwenye hotuba yake juzi kwamba tusitafute mchawi wala sio wakati wa kulaumiana. Mimi nakubali kwamba huo si wakati wa kulaumiana bali wa kuwajibishana,” alisema Lissu.
Alionesha ripoti ya serikali ya mwaka 2010 iliyochunguza chanzo cha kufeli kwa matokeo ya kidato cha nne, lakini haijafanyiwa kazi wala haijatangazwa hadharani.
“Ripoti hii Waziri Mkuu anaijua, hajaifanyia kazi, leo ameunda tume nyingine. CHADEMA tunasema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi afukuzwe, Waziri Mkuu afukuzwe, wameshindwa kazi,” alisema.
Alisema kama rais hataki kumwajibisha, Bunge lipige kura ya kutokuwa na imani naye.
Baada ya Lissu kumaliza kujadili hoja hiyo, Spika Makinda aliitaka Kamati ya Kanuni kukutana kwa dharura kujadili ukiukwaji huo wa kanuni mpya walizojiwekea, na hivyo kufikia hatua ya wabunge kujadili jambo lililoko mahakamani.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More