Jumatatu, 8 Aprili 2013

Njama za kuvuruga kuapishwa kwa Uhuru Kenyatta

Polisi waonya dhidi ya njama zozote za kuvuruga sherehe za Jumanne za kumwapisha rais wa nne wa Kenya.

 Polisi  wa Kenya wamewataka  baadhi ya watu kuripoti kwa mkuu ya kitengo cha upelelezi (CID) bwana Nicholas Kamwende kufuatia tuhuma kwamba wanapanga njama za kuvuruga sherehe za kumwapisha bw. Uhuru Kenyatta kama rais wa nne wa Jamhuri ya Kenya siku ya Jumanne.

Inspekta Jenerali wa polisi David Kimaiyo amesema Jumapili kuwa kundi la vijana linapanga maandamano katika maeneo mbalimbali ya Nairobi ambayo hatimaye yatageuka kuwa ghasia wakati wa sherehe hizo za Jumanne.

Bw. Kimaiyo ameviambia vyombo vya habari vya Kenya kuwa polisi wana taarifa kwamba bw. Jeckonia Junga Onyango, aliandaa mkutano na kukamilisha mpango wa njama hizo katika eneo la mabanda la Kibera nje kidogo ya Nairobi.

Taarifa za polisi huko Nairobi zinasema miongoni mwa maeneo yanayopangwa kufanyika maandamano hayo ni pamoja na Kibera, Kangemi, Kamukunji, Dandora na kariobangi.Vijana hao yaripotiwa wamepanga  kupora mali kuchoma mali na hata kushambulia wapinzani wao huku wakiwa na silaha kama vile mapanga. Bwana Kimaiyo ameonya kuwa uhalifu wa aina yoyote hutavumiliwa nchini humo.

Habari zaidi zasema waziri mkuu anayeondoka madarakani na ambaye alishindwa katika kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi uliopita bw. Raila Odinga amekwenda Afrika Kusini kwa mapumziko.Taarifa kutoka kwa msemaji wake Dennis Onyango zinasema  bw. Odinga hataweza kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mteule Uhuru Kenyatta Jumanne licha ya mwaliko rasmi wa kuhudhuria sherehe hizo.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More