RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
Ludovick Utouh, imewasilishwa bungeni huku ikiendelea kueleza madudu
mengi yaliyopo serikalini. Ripoti hiyo, inayoishia Juni 2012,
iliwasilishwa jana kisha ikatolewa ufafanuzi na CAG mwenyewe, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari.
Katika mazungumzo yake, CAG, ambaye alikuwa ameambatana na Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Serikali Kuu (PAC), Zitto Kabwe na Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Serikali za Mitaa (LAAC), Rajab Mbarouk Mohamed,
alionyesha jinsi fedha za umma zinavyoendelea kutafunwa, licha ya hati
zenye shaka kupungua katika halmashauri nchini.
Wakati wa ukaguzi
huo kwa upande wa Serikali za Mitaa, alisema vitabu 2,990 vya
stakabadhi za mapato kutoka katika halmashauri 36 havikuonekana na
kwamba halmashauri 22, kati ya 134 zilizopo nchini, zililipa Sh bilioni
1.5 ambazo hazikuwa na hati za malipo.
Alisema malipo yenye hati pungufu, yalibainika katika halmashauri 74
ambayo jumla yake ni Sh bilioni 3.3 na kwamba jumla ya Sh milioni
650.3, zililipwa katika halmashauri 20 kwa ajili ya taasisi mbalimbali
zilizoko vijijini, ingawa fedha hizo hazikufika zilikokusudiwa.
“Pamoja
na hayo, jumla ya Sh milioni 693,132,772, zililipwa kama mishahara kwa
wastaafu, watoro, watumishi waliofariki, watumishi walioacha kazi au
walioachishwa kazi kupitia akaunti zao na malipo hayo yamehusisha
halmashauri 43.
“Kutokana na kuwepo kwa kiwango cha chini cha
uzingatiaji wa taratibu na sheria za manunuzi, kulisababisha manunuzi
yenye thamani ya Sh milioni 443,107,149 kufanyika katika halmashauri 25
na pia bidhaa zenye thamani ya Sh milioni 541,013,405 ulifanyika bila
kibali cha bodi ya zabuni katika halmashauri 24,” alisema CAG.
0 maoni:
Chapisha Maoni