Maranyingi katika maisha yetu ya
kilasiku tumesikia sana maneno kama “nipe tano” “chukua tano” maneno haya
yamekuwa maarufu sana na katika mazingira tofauti maneno haya yamekuwa
yakiashiria ushindi, au hali ya mafanikio au furaha baada ya hali fulani. Vivyo
hivyo katika maisha yetu ya kutafuta kufanikiwa katika yaleyote tunayoyafanya
kilasiku viko vitu au ziko hatua ambazo huwa zinatulazimu kuzijua au kuzipitia
kama kweli tunamaanisha na tunayadhamiria hayo mafanikio tunayoyatafuta. Ni
ukweli kwamba watu wengi hutamani sana mafanikio na kuyazungumzia sana katika
maneno yao ya kilasiku lakini kwa bahati mbaya hawajawahi kuyaishi mafanikio
hayo kwasababu ya kutokuwa na dhamira madhubuti katika kuyaelekea mafanikio
hayo. Kama ambavyo tunaposema “high five” tunagonga mikono yetu na vidole vyetu
vitano vikiwa vimefunguka kuashiria ushindi basi vivyohivyo nitajaribu kugusia
hatua tano au vitu vitano vitakavyokusaidia kugonga mkono wa “ high five” baada
ya kuyafikia mafanikio yako. Kwakifupi vitu hivyo ni, Uwezo binafsi wa
kuvikagua vile ulivyo navyo ndani yako, uwezo wa kusimama au kuwa na msimamo,
uwezo wa kupiga hatua, uwezo wakujitengenezea sura ya maisha yako, na uwezo wa
kuyaongoza maisha yako. Fuatana na mimi katika kuzichambua hatua hizi hapa
chini.
1. 1. Kuwa na uwezo binafsi wa
kuvikagua vile ulivyonavyo ndani yako (Take a stock)
Katika maisha yetu ya kilasiku
hatunabudi kujifunza namna ya kujikagua sisi wenyewe, kuvikagua vile
tulivyonavyo ndani yetu kwasababu ni ukweli kwamba pasipo kujikagua sisi
wenyewe basi hatutaweza kuyatambua mapungufu tuliyonayo na kama hatutoyatambua
mapungufu tuliyonayo basi mapungufu hayo hayatoweza kushuhulikiwa na
kuondolewa, maana yake ni kwamba tutazidi kuishi na mapungufu yetu na hivyo
kuathiri ufanisi wetu na mwisho wake mafanikio yetu kwa ujumla yataathirika.
Labda nikupe mfano wa mtu mwenye duka, mara kwa mara mmiliki wa duka huwa na
muda wa kuvikagua vitu au mali aliyonayo dukani (stock taking) na hapa
huwezakutambua nini kimepungua, nini hakipo kabisa na nini kipo kwa wingi.
Katika kujikagua sisi wenyewe sio tu tunapata uhakika wa vile tusivyonavyo
(weaknesses) bali pia tunapata kufahamu vile tulivyonavyo kwa wingi (strengths).
Jifunze kufanya tathmini ya maisha yako binafsi kila wakati, tathmini matendo
yako ya kilasiku, maneno yako ya kilasiku, mitazamo yako (perceptions and
attitudes) halafu angalia wapi kuna mapungufu na wapi kuna fursa zaidi). Baadhi
ya mapungufu ambayo twaweza kuwa nayo katika maisha ni kama vile mapungufu ya
kihisia (emotional gaps), mapungufu ya kiroho (spiritual gaps), mapungufu ya
kiujuzi (skills gaps), mapungufu ya kifedha (financial gaps) na mengineyo
mengi. Kumbuka, uzuri ni kwamba kila tunapoweza kuyatambua mapungufu haya
tunaziona fursa za kuweza kuyashuhulikia.
2. 2. Uwezo wa kuwa na msimamo (Take a
stand)
Wengi wetu tumeshindwa kuyafikia
malengo tuliyowahi kujiwekea kwasababu tu hatunamisimamo katika vile
tunavyoviamini kwahiyo inakuwa rahisi kuyumbishwa na kupeperushwa na kila upepo
unaokuja upande wetu. Ili kufikia mafanikio tunayoyatamani hatunabudi kuwa na
misimamo fulani katika maisha. Naupenda msemo unaosema kama huwezi kuwa
na msimamo katika chochote basi utachukuliwa na chochote “He who stands for
nothing will fall for anything”. Kama wewe ni kijana na huna msimamo katika
chochote basi ni rahisi kujikuta unachukuliwa na vingine ikiwemo madawa ya
kulevya, umalaya n.k. Kama wewe ni mfanyakazi na hauna msimamo katika baadhi ya
mambo basi ni rahisi kujikuta unabebwa na mengi kama vile rushwa na ubadhilifu.
Ni vema kufahamu kila wakati maishani kuwa kama hauna msimamo katika ufanisi
basi utaangukia katika uzembe na kutowajibika, na kama hautakuwa na msimamo
katika kuhakikisha unafanikiwa basi utaangukia katika umaskini.
Kusimamia kitu fulani
maanayake ni kuwa na nidhamu, kujua kanuni, na kukiheshimu kitu kile
unachokisimamia. Kanuni na nidhamu hizi ndizo zinazotuongoza katika maisha yetu
ya kilasiku katika kufikia kile tunachotamani. Amua mwenyewe ninini unasimamia
na ni wapi unaiweka misimamo yako kwasababu vile tunavyoamua kuwa na misimamo
navyo ndivyo vinavyosimama kama misingi katika maisha yetu.
- Uwezo wakupiga hatua (Take a step)
Yamkini unatamani sana kufanikiwa na
kilasiku unaongelea sana mafanikio, ni vema kujua kwamba mafanikio yetu hayaji
kwa kuyatamani sana au kuyaongelea sana bali katika uwezo binafsi wa kuamua
kupiga hatua. Yawezekana uko katika chombo kizuri tu cha usafiri lakini
utajikuta unapitwa na kila mtu, hata wale wenye vyombo vibovu vya usafiri nao
watakupita kama utakuwa umekaa tu kwenye chombo chako pasipo kuruhusu mwendo.
Chukua hatua kuelekea mustakabali wako, angalia mbele yako unaona nini? nini
ambacho unakiona kwenye mustakabali wako? Nini ungetamani ukipate kwenye
mustakabali wako? Anza kufanya kila kinachohusika ili kuiona hiyo ndoto yako
ikiwa dhahiri. Anza kupiga hatua ya kwanza na hatua nyingine zitakuwa rahisi
kufuatia. Kamwe usitishike na umbali unaouona kuelekea mustakabali wako, jinsi
unavyopiga hatua ujasiri wako unafunguka na kukua, kumbuka kuwa kila hatua
unayoipiga hatakama nindogo kiasi gani inakusogeza karibu na mustakabali wako.
Usisahau tu kuwa ziko mbio unatakiwa kuzikimbia na uko ushindi unatakiwa
kuushinda ilikufikia hapo unapotamani, kwahiyo piga hatua.
- Uwezo wa kujitengenezea sura ya maisha yako (Take a shape)
Katika maisha yetu ya kilasiku ni
ama uamue kuitengeneza sura ya maisha yako au kuibomoa sura hiyo, wengine wetu
maisha yetu hayajawahi kuwa na sura nzuri ya kuvutia, sisi wenyewe ndiyo
wenyeuwezo wakuamua kuitengeneza sura hiyo kuwa vile tunataka iwe, ukiamua
kukaa tu pasipo kufanya chochote basi umekusudia kwa dhamira halisi kuiharibu
sura ya maisha yako mwenyewe. Ulimwengu waleo unabadilika kwa kasi sana, ili
kuweza kubakia wenye maana na wenye umuhimu basi hatuna budi kuwezana na
mabadiliko hayo. Kama hatutoweza kuyaweza mabadiliko ya karne hii basi
mabadiliko hayo yatatuweza sisi (If you don’t manage change change will
mismanage you). Fahamu dhahiri kwamba karne ya 21 haijaleta tu fursa bali
na changamoto tele.
Lazima tuweze na tuwe na ujuzi wa
kufanya tabia zetu za kilasiku kuendana na mabadiliko haya, lazima kuwa kasi
kama vile kasi ya mabadiliko ilivyo, lazima kuwa wenye uwezo wa kuendana na
mazingira kwasababu ukijaribu kukakamaa na kutokubali mabadiliko (being rigid)
katika enzi hizi basi lazima utavunjika. Chamsingi wote tujitahidi kufanya hata
yale ambayo maranyingine hayaturidhishi sana, yale ambayo tunaona yanatugarimu
zaidi na kutuminya zaidi, kumbuka mafanikio sio wakati wote yanakuja tukiwa
tunayasubiria kwa kicheko bali maranyingine kwa kuumia (we must be willing to
step out of our comfort zones)
- Uwezo wa kukikalia kiti na kuyaongoza maisha yako mwenyewe (Take a seat)
Ziko nyakati ambazo wengi wetu
hatuwezi kufika tunapotamani kufika kwasababu dereva anayeendesha chombo chako
sio wewe, wakati huohuo unafikiria kuelekea pale unapotamani wewe. Ningumu
sana. Katika maisha kama kweli unaifahamu ndoto yako na unaiona kesho yako na
unaitamani sana kuifikia basi amua kukaa kwenye kiti cha dereva wewe mwenyewe
na kuendesha chombo kuelekea huko. Wengi wetu sio kwamba tumewakabidhi wengine
udereva wa safari yetu kwa kujua bali kwa kutokujua, mara unaona muelekeo wa
safari sio ule ulioutarajia, yamkini sasa dereva uliyemkabidhi kiti anakupeleka
kwenye ndoto yake siyo yakwako tena. Sasa amuakuingia kwenye kiti cha dereva
wewe mwenyewe, hayo ni maisha yako na siyo ya mwingine. Kamwe usiache furaha na
mafanikio yako katika mikono ya wengine. Kubali na kuwa tayari kubeba majukumu.
Kama inatokea unafanya makosa basi usijitetee na kukwepa, kwasababu kujitetea
na kukwepa yawezakuwa njia tu ya kuchomoka na siyo njia ya kuendelea mbele.
Usiwalaumu wengine kwa madhaifu na kushindwa kwako, kwasababu kwa kufanya hivyo
unaipoteza nguvu ya kukua.
Chukua tano!!!!
Acknowledgement:
Dr John Tibane’s teachings.
Prepared
by Chris Mauki
Social and
counseling psychologist
PhD
candidate, University of Pretoria
South
Africa
0 maoni:
Chapisha Maoni