SHIDA Salum, mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia
na Maendeleo
(CHADEMA), Zitto Kabwe, amenusurika kuuawa baada ya
kuvamiwa nyumbani kwake na watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi,
wakiwa na silaha za moto.
Habari zilizolifikia MTANZANIA Jumatano kutoka kwa watu walio karibu
na mama huyo zilieleza kuwa, vijana hao walifanikiwa kumfikia akiwa
katika sebule ya nyumbani kwake na kumuelekezea bastola kichwani, huku
wakimlazimisha awakabidhi baadhi ya vifaa vyake vya kufanyia kazi na
simu yake ya kiganjani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, tukio hilo lilitokea Ijumaa ya Aprili 19, majira ya saa moja na nusu asubuhi.
Akizungumza
na MTANZANIA Jumatano kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu tukio hilo,
mama yake Zitto alisema ni kweli lilitokea na amekwisharipoti katika
kituo cha Polisi cha Buguruni.
Mama Zitto alisema siku kadhaa
kabla ya tukio hilo alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa
mwanachama wa Chadema wa Tawi la Tabata Relini na kumuomba msaada wa
mifuko miwili ya saruji kwa ajili ya kukarabati jengo la ofisi yao.
Alisema
alikubali kuwasaidia vijana hao kwa kuwataka wafike nyumbani kwake
mapema siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, kwa sababu alikuwa na ratiba
ngumu na ndefu siku hiyo.
“Nilikubaliana nao hivyo, bila kuwa na
fikra kwamba wanaweza kuwa watu wabaya, hivyo walipokuja nyumbani kwangu
baada ya kuruhusiwa na mlinzi niliwakaribisha ndani na kuwaeleza kuwa
nitawapatia Sh 20,000 na Sh10,000 waongeze wenyewe.
“Lakini
niliposimama kuelekea chumbani kuwachukulia kiasi hicho cha fedha, mmoja
wao alitoa bastola na kunielekezea kichwani huku akieleza kuwa hawana
shida na pesa, bali wanataka laptop yangu, flash na simu yangu ya
mkononi kwa sababu zina mambo muhimu,” alisema mama Zitto.
Alieleza
zaidi kuwa alipowauliza ni kwa nini wanataka vitu vyake hivyo,
walieleza kuwa anajua sababu na hata siri yake ya kutumia nafasi yake ya
uongozi wa chama cha walemavu kuzunguka nchi nzima akimnadi mwanaye
Zitto kwa wana Chadema kuwa anafaa kuwa mwenyekiti wa chama hicho na
rais wa Tanzania inafahamika.
“Nilijua kuwa ninakufa, sikuona
haja ya kubishana nao sana, nikamwita dereva wangu, Mtana, alete simu
yangu niliyokuwa nikiichaji chumbani na flash ili niwapatie, wakati
akielekea kuvichukua aliwaona walivyokuwa wameniwekea bastola, akakimbia
moja kwa moja chumbani akajifungia na kuanza kupiga kelele, wakatoka
haraka wakakimbia,” alisema.
Alipoulizwa iwapo hawakupata
upinzani wowote kutoka kwa mlinzi aliyekuwa getini au majirani
walishtushwa na kelele za dereva wake, alisema wakati wanatoka geti
lilikuwa wazi na mlinzi alikuwa akiosha gari nje, hivyo ilikuwa rahisi
kutoka na gari lao na kutokomea.
Alisema anaweza kuwatambua watu
hao akiwaona na kwamba mmoja wao si mgeni machoni mwake, kwa sababu
aliwahi kumuona mkoani Tanga katika moja shughuli za chama hicho.
Mama
Zitto alieleza zaidi kuwa kabla ya tukio hilo, amekuwa akiulizwa na
baadhi ya wafuasi wa chama na hata watu wengine mahali anakopata fedha
za kuzunguka mikoani kumnadi mwanaye, Zitto kwa ajili ya kugombea urais
na uenyekiti wa chama.
Alisema kwa sababu ya kuhofia maswali
ambayo amekuwa akiulizwa mara kwa mara, alimfikishia taarifa Kaimu
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Ahmed Sagula, lakini katika
hatua ambayo hakuitegemea, naye alimhoji mahali anakopata fedha za
kuzunguka mikoani kumnadi Zitto, kabla ya kumuahidi kushughulikia
malalamiko yake.
Sagula mwenyewe hakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake kutopatikana kila ilipopigwa.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, naye hakuweza
kupatikana kuzungumzia suala hilo na hata Mkuu wa Kituo cha Polisi
Buguruni, mahali ambako Mama Zitto ameripoti tukio hilo naye hakuweza
kupatikana.
0 maoni:
Chapisha Maoni