Jumatatu, 29 Aprili 2013

Yanga ijipange kwa mashindano ya Afrika

Timu ya soka ya Yanga ndiyo mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2012/2013.
Yanga imetwaa ubingwa huo ikiwa bado imebakiza mechi mbili ambazo ni dhidi ya Coastal Union na Simba.
Huu ni ubingwa wa 24 kwa Yanga tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu Tanzania Bara rekodi ambayo hakuna timu yoyote ya Tanzania inayoifikia kwani Simba wanaowafuatia wametwaa ubingwa huo mara 18 tu.
Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992,1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2007-2008, 2008-2009, 2010-2011 na 2012-2013.
Kwa ubingwa wa Ligi Kuu iliyotwaa Yanga imepata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya klabu bingwa Afrika mwakani.
Historia ya soka la Tanzania inaonyesha kuwa kabla mashindano hayo ya Afrika hayajaitwa Ligi ya Mabingwa kutoka klabu bingwa Afrika, timu ya Simba ndiyo iliwahi kufika hatua ya nusu fainali.
Tangu mashindano hayo yabadilishwe jina mwaka 1997 na kuitwa Ligi ya Mabingwa barani Afrika timu za Simba na Yanga zote zimewahi kuishia hatua ya makundi tu.
Tunaamini Yanga ambayo itatuwakilisha mwakani katika mashindano ya klabu bingwa ya Afrika ina jukumu kubwa la kuipeperusha bendera ya Tanzania.
Yanga itaweza kufanya vizuri katika mashindano hayo kama viongozi wao watakuwa na malengo ya kutaka kutwaa ubingwa wa Afrika na kucheza mashindano ya FIFA ya klabu bingwa ya dunia.
Tunasema hivyo kwa sababu ili kutwaa ubingwa wa Afrika, lazima kuwe na mipango madhubuti ya kufanikisha hilo ambayo ni usajili mzuri, maandalizi mazuri na kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya mashindano hayo ya Afrika.
Viongozi wa Yanga wanatakiwa kufanyia kazi ripoti watakayopewa na kocha wao mwisho wa msimu huu ili wajue kikosi chao kina mapungufu gani na wafanye vipi usajili utakaowawezesha kuwa na kikosi chenye wachezaji mahiri wanaoweza kupambana katika mashindano hayo makubwa ya Afrika.
Tunasema hivyo kwa sababu tumeshuhudia mechi nyingi za mashindano hayo ya Afrika na kuona jinsi klabu za wenzetu zilivyo na wachezaji wenye akili ya mchezo, miili ambayo imefanyishwa mazoezi kwa ajili ya kupambana uwanjani ili kupata ushindi na stamina.
Tumeona pia katika mashindano hayo ya Afrika jinsi wachezaji wa timu mbalimbali wanavyotoa pasi na kupokea mpira, kufunga mabao, kuzuia, kushirikiana, kukokota mpira, kupiga mashuti, kuusoma mchezo kwa haraka, kujiamini na wachezaji kufanya uamuzi wa haraka.
Vilevile Yanga inaweza kufanya vizuri katika mashindano hayo ya Afrika kama wachezaji watakuwa na umoja, bidii na kuwa na lengo moja la kutafuta ushindi, pia wachezaji wachezaji wanatakiwa kujiandaa wenyewe kwa kufanya mazoezi binafsi.
Tunatarajia kuona Yanga ikitumia kipindi hiki vizuri kwa ajili ya kujiandaa na mashindano hayo ya klabu bingwa Afrika ili kufuta aibu ya kuishia hatua ya pili kila wakati.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More