Nairobi. Rais mpya wa Kenya, Uhuru Kenyatta
amefungua rasmi Bunge la nchi yake kwa kutangaza vita dhidi ya rushwa
ambayo imekithiri katika idara nyingi za Serikali.
Akizungumza kwa kujiamini kwenye Ukumbi wa Bunge
uliokarabitiwa hivi karibuni, Kenyatta alieleza kwamba hivi sasa
anaandaa safu ya mawaziri makini watakaomsaidia kuendesha Serikali yake
na watakaohakikisha anatimiza agenda zake muhimu.
Katika hotuba yake kwa wabunge na maseneta jijini
Nairobi, Kenyatta alisema kwamba suala la rushwa limekuwa kikwazo katika
utoaji huduma.
Kenyatta pia alitaja vipaumbele vinane muhimu
katika Serikali, ambavyo ni kuhakikisha kunakuwepo uwazi katika utoaji
wa huduma za jamii, kuzalisha nafasi za ajira, elimu, ulinzi, kuboresha
miundombinu na kuwa na Serikali itakayosaidia kuimarisha umoja wa
kitaifa.
“Serikali yangu pia itasimamia sheria ipasavyo
ikiwamo kuwasilisha miswada bungeni na kusimamia utekelezaji wa Katiba
Mpya ya nchi hiyo.
“Pia suala la usalama ni muhimu sana, tunatakiwa
kuongeza idadi ya polisi, kuwajengea uwezo wa vifaa na kuboresha
masilahi yao,” alisema Kenyatta.
Katika suala la elimu, Kenyatta alisema wanafunzi
wote watakaoanza darasa la kwanza mwaka kesho na wale wanaoingia vyuo
vya elimu ya juu watapatiwa kompyuta pakatwa (laptop).
Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake alizotoa wakati wa kampeni iliyompa ushindi.
Alieleza kwamba vyuo vya elimu ya juu pia
vinatakiwa viongezwe kwenye kaunti zote ili kuzuia vyuo vya elimu ya
kati kutumika kama vyuo vikuu.
Katika suala la ajira, Uhuru alieleza kwamba upo
umuhimu wa kuwawezesha vijana na wanawake kupata ajira, mfuko maalumu
umeanzishwa, ambapo fedha za miradi zitatakiwa kupelekwa kwenye ngazi ya
majimbo.
Kenyatta alisema kwamba kwa sasa upo umuhimu wa
kuangalia zaidi kwenye mapinduzi ya viwanda na kuhakikisha kwamba
wanaandaa na kuboresha bidhaa za ndani.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
0 maoni:
Chapisha Maoni