Dar es Salaam. Mabweni ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wazo Hill nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, yameteketea kwa moto na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.
Moto huo uliozuka mapema asubuhi, inadaiwa ulisababishwa na hitilafu ya umeme.
Akizungumza jana shuleni hapo, mmiliki wa shule
hiyo, Valence Msaki alisema moto huo ulianza saa 11 asubuhi wakati
wanafunzi wakiwa kwenye mazoezi ya viungo.
Alisema ulianzia kwenye chumba cha viongozi wa
mabweni na licha ya kuwa haukuleta madhara kwa binadamu, lakini
umesababisha hasara ya mali mbalimbali za wanafunzi vikiwemo nguo,
madaftari, vitanda na magodoro.
Msaki alisema mlinzi aligundua moto huo alipokuwa anakagua mabweni hayo kwani aliona ukitokea kwenye chumba cha viongozi.
Alisema ni asilimia 40 tu ya wanafunzi hao waliokoa baadhi ya vitu vyao na asilimia 60 hawakufanikiwa, hivyo vimeteketea.
“Moto huu ulianzia kwenye chumba wanacholala
viongozi wa bweni inawezekana ikawa chanzo ni hitilafu ya umeme kwa kuwa
chumba hicho muda wote taa huwa hazizimwi,” alisema Msaki.
Msaki alisema magari ya Kikosi cha Zimamoto
yalifika saa 2.30 asubuhi, huku juhudi kubwa za kuuzima moto huo
zikifanywa na wananchi, walimu na wanafunzi ambao walitumia maji,
mchanga na baadhi ya vifaa vya kuzimia moto vya shule hiyo.
“Sasa hivi tunajipanga ili watoto waweze kulala na
kesho tutafanya tathmini ya vitu vilivyoungua ili tujue vitu vingapi
vimeungua,” alisema Msaki.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles
Kenyela alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema: “Kizuri ni
kwamba hakuna vifo wala mtu aliyejeruhiwa.”
Aliwataka wakuu wa shule mbalimbali katika mkoa
huo kufanyia ukaguzi vifaa vya moto na kuziweka shule zao katika hali ya
tahadhari ili kusitokee maafa pindi inapotokea ajali za moto.
Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Samueli Nainda
alisema kwamba wanaiomba Serikali iwasaidie kutokana na hasara
iliyosababishwa na moto huo.
CHANZO: Mwananchi
CHANZO: Mwananchi
0 maoni:
Chapisha Maoni