JESHI la
Polisi Makao Makuu limeendelea kumshikilia kwa siku 11 bila kumfikisha
mahakamani Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) mjini
Bukoba, Evodius Justinian (30) huku ndugu zake wakizuiliwa kumpa chakula
isipokuwa maji tu.
Justinian
alishikiliwa mjini Bukoba Aprili 2, mwaka huu kisha kusafirishwa hadi
jijini Mwanza na kuhojiwa, kisha Dar es Salaam huku akipewa mateso
makali ya kulazimishwa akubali kuhusika kutengeneza video inayomhusisha
na uchochezi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred
Lwakatare.
Awali ndugu
zake na viongozi wa CHADEMA mjini Bukoba walielezwa na polisi kuwa
Justinian anasafirisha kwenda wilayani Igunga, Tabora ambako alidaiwa
kuwa alitenda makosa ya jinai, lakini alifichwa jijini Mwanza.
Wakizungumza
na gazeti hili, mawakili wa mtuhumiwa huyo Nyaronyo Kicheere na Peter
Kibatala walisema kuwa juzi jioni ndugu zake walimpelekea chakula,
lakini walipofika waliambiwa kuwa haruhusiwi chakula isipokuwa maji tu.
“Asubuhi
alipelekewa chai, lakini polisi walidai kuwa ndugu walichelewa na hivyo
kuwazuia. Na walipopeleka chakula cha mchana waliambiwa hayupo kwani
alikuwa amepelekwa hospitali bila kuitaja kwa jina,” alisema Kicheere.
Kicheere
aliongeza kuwa baada ya ndugu kuwapa taarifa hiyo, yeye na wakili
mwenzake Kibatala walilazimika kuondoka mahakamani Kisutu walipokuwa
wakimsubiri mteja wao afikishwe.
Mawakili hao
walisema wanakusudua wakati wowote kupeleka maombi Mahakama Kuu kudai
polisi wapeleke mwili wa mtuhumiwa mahakamani (habeas corpus).
Lakini pia mawakili hao walisema kuwa leo wataendelea kushinda mahakamani muda wote wa kazi kumsubiri mteja wao.
Waliwataka
Watanzania wakiwemo wanasheria na watetezi wa haki za binadamu kuendelea
kupiga kelele dhidi ya Jeshi la Polisi linavyokiuka haki za binadamu.
Akizungumzia
hatua ya mtuhumiwa huyo kutofikishwa mahakamani kama ilivyokuwa
imeahidiwa, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso alisema wakiwa
tayari watasema na kuomba watu wasiingilie kazi yao.
“Tutasema
siku ya kumfikisha, hapa suala la msingi ni polisi tunafanya nini, ni
kama wewe unavyoandika habari, hakuna wa kukuuliza,” alisema Senso.
Alipoelezwa
juu sheria inavyotaka mtuhumiwa kufikishwa mahakamani ndani ya saa 24
baada ya kukamatwa, Senso alisema pasipo kufafanua kuwa sheria hiyo hiyo
inaweza kutumika vinginevyo.
Jumatatu
wiki hii, mbele ya wakili wake Kicheere, mtuhumiwa huyo alieleza unyama
aliofanyiwa na jeshi hilo wakati wote wa mahojiano mkoani Mwanza na
jijini hapa.
Katika
maelezo yake yaliyoshuhudiwa na Ofisa wa Polisi Makao Makuu, Advocate
Nyombi, Justinian alisema kuwa baada ya kutolewa mjini Bukoba kwa siri
bila ndugu zake kujua, alipelekwa jijini Mwanza na kuhojiwa bila
kuruhusiwa kuonana na wakili wake.
Alieleza
kuwa wakati wote wa mahojiano hayo alikuwa akilazimishwa kukiri kurekodi
video ya Lwakatare inayoonesha mikakati ya ugaidi.
Alisema
alisafirishwa kwa siri kwa ndege hadi Dar es Salaam, akapelekwa chooni
na kupigwa, kutishiwa na kuteswa kwa nyaya za umeme na kunyimwa fursa ya
kupewa chakula.
“Nimepigwa
na polisi nikiwa Mwanza, nikiwa chooni Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam
wakati naletwa huku, polisi wakaniambia mimi ni mtu hatari sana, niseme
nilifanya nini Igunga.
“Nikiwa
Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam niliomba kwenda chooni, waliingia
pamoja na mimi wakanipiga sana, nimeshaandika maelezo kwa kulazimishwa,
niliomba kuwa na wakili wakanikatalia,” alisema.
Aliongeza
kuwa akiwa Dar es Salaam alihojiwa aseme ukweli kuhusu video ya
Lwakatare. Akawajibu kuwa ilifanyiwa uhariri na Ludovick, lakini
akapigwa makofi na askari wakaagiza nyaya za umeme za kutesea.
“Waliposema kuleta nyaya za umeme, kwa kuhofia mateso ya umeme nikasema hii video ni yangu,” alisema.
0 maoni:
Chapisha Maoni