Jumatano, 10 Aprili 2013

DPP Zanzibar akata rufaa.



Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim amekata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania, akipinga maamuzi ya Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Fatma Hamid Mahmoud ya kumpa wiki mbili kueleza kwa maandishi sababu ya kufunga dhamana ya viongozi wa Jumuiya ya Uamsho.

Msimamo wa DPP, umewasilishwa Mahakamani Jumatano, Mwanasheria wa Serikali Raya Mselem, ambaye ameitaarifu Mahakama Kuu kuwa taratibu ya kufungua rufaa imekamilika, hivyo haoni haja ya kuwasilisha maelezo kama alivyotakiwa na Jaji Fatma April tano ,mwaka huu.

Hata hivyo, Wakili wa upande wa utetezi, Salum Tawfiq amesema kwa kuwa suala hilo lilikuwa ni amri ya mahakama, upande wa mashtaka walitakiwa kueleza nia yao ya kukata rufaa baada ya uamuzi huo kutoka badala ya kukaa siku zote na kuja na hoja hiyo siku ambayo DPP alitakiwa kuwasilisha maelezo hayo.

Tawfiq amesema wateja wake wamekuwa kizuizini kwa muda mrefu na kumuomba Jaji Fatma Hamid Mahmoud kuzingatia ombi lao la dhamana, licha ya Mkurugenzi wa Mashtaka kufungua ombi lake Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Kwa upande wake, Jaji Fatma Hamid Mahmoud amesema kwa mujibu wa sheria, maamuzi yanayosubiri Mahakama ya juu, kesi ya msingi katika Mahakama ya chini italazimika kusimama hadi hapo Mahakama ya Rufaa ya Tanzania itakapotoa maamuzi yake.

Aidha, Jaji Fatma amesema kesi ya msingi itaendelea tena baada ya siku 60, wakati maombi mawili ya rufaa yatakapotolewa uamuzi na Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Maamuzi yaliyokatiwa rufaa katika Mahakama ya Rufaa Tanzania, na Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar(DPP) Ibrahim Mzee Ibrahim ni maamuzi ya Jaji Abraham Mwampashi ambaye alifuta maamuzi yote ya Mrajis wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, ikiwemo kuungana na uamuzi wa DPP wa kuwanyima dhamana viongozi wa Uamsho.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More