Jumapili, 28 Aprili 2013

Wafu wanavyofukuliwa, kisha kuzikwa wapya

 Siku zote tunaamini kuwa mtu anapofariki hupumzika kwa amani, lakini siku hizi wafu hao hawapumziki tena kwa amani, bali huamshwa, kisha, wafu wengine kushika nafasi zao.
Ni kama vile muda wa marehemu hao kukaa kaburini umekwisha hivyo, nafasi zao zinatakiwa kutumiwa na wengine kutokana na uhaba wa maeneo ya kuzikia.
Maeneo mengi ya kuzikia katika Jiji la Dar es Salaam, hasa yale maarufu kama Kinondoni, Sinza, Temeke na Kisutu yanapendwa zaidi na watu na sasa yamefurika.
Kujaa kwa maeneo haya ya kuzikia kumesababisha makaburi ya watu wengine, kufukuliwa kisha kutumika kuzikia miili mingine.
Hata hivyo, makaburi ambayo hufukuliwa ni yale ambayo hayajajengewa, yametelekezwa, hayana kitu chochote cha kuonyesha kuwa kuna kaburi pale au mengine hayana alama kama misalaba au imeondolewa.
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni, Sebastian Kaiohela anasema kuwa anafahamu kwamba makaburi hayo yamejaa, lakini hakutaka kuzungumza zaidi akitoa ahadi kuwa siku ya Jumatatu atalifikisha suala hilo kwa wahusika wakuu.
Katika makaburi ya Temeke Chang’ombe, Mwananchi Jumapili lilishuhudia makaburi yakiwa yamesongamana kiasi ambacho ni vigumu mtu kupata nafasi ya kuweka mguu.
Mlinzi wa makaburi hayo, Athuman Mtembwe anasema kutokana na ufinyu wa nafasi katika makaburi hayo, makaburi ambayo hayana alama yoyote ni rahisi kufukuliwa na kuzikiwa kwa mara nyingine.
“Mimi kama mlinzi wa eneo hili ninaweza kukutafutia sehemu ambayo unaweza kuchimba kaburi, lakini kama hufahamu utafukua tu maiti nyingine,” anasema
Anasema kuwa mara kwa mara watu wanaokuja kuchimba makaburi ili kuzika ndugu zao, wamekuwa wakifukua miili ya watu wengine ambayo makaburi yao hayakuwa na alama yoyote.
“Ni kawaida, mchimba kaburi anafukua, anakuta mifupa, anaiweka pembeni au anaizika katika shimo dogo…kisha anaendelea na taratibu za kuzika mwili mwingine,” anaeleza.
Lakini Mtembwe anasisitiza kuwa iwapo atachimba yeye, hawezi kufukua kaburi lililokwishatumika kwani anafahamu maeneo machache ambayo hayajatumika, ingawa ni finyu mno.
“Hapo uliposimama ni kaburi hapo ingawa wewe hujui,” anasema akimwambia mwandishi wa makala haya huku akimwonyesha kwa kidole kuwa aliposimama ingawa hakuna dalili ya kuwepo kwa kaburi, lakini lipo.
Mzee Mtembwe ambaye amekuwa mlinzi wa makaburi hayo kwa zaidi ya miaka 30, anaeleza kuwa siyo kwamba ardhi ya kuzikia hakuna kabisa, bali hali hiyo inatokana na tabia ya watu kupenda kuzika karibu au mahali ambapo ndugu wengine wamezikwa.
“Maeneo mengine ya kuzikia yametengwa, huko Yombo Buza na Tabata Segerea, lakini wanaoyatumia ni wale wanaoishi huko au ambao hawaoni umuhimu wa kuzikia hapa Temeke,” anasema.
Anasema imejengeka dhana kwa jamii kupenda kuzikia maeneo ya Sinza, Kinondoni au Temeke.
Anaisihi jamii kuwa inapomzika ndugu au rafiki, isikawie kujengea au kuweka alama ya kudumu, vinginevyo ni rahisi watu kutumia tena eneo hilo kwa kuzikia.
Hata hivyo, jitihada za gazeti hili za kuwatafuta wakurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Kinondoni na Ilala ili kuzungumzia adha hii hazikufanikiwa.
Lakini, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Mecky Sadiki alisema anafahamu kuwa watu wengi wanapenda kutumia makaburi maarufu kama Kinondoni, Temeke na Sinza, licha ya maeneo hayo kujaa.
“Makaburi hayo yanapendelewa zaidi kwa sababu labda ya ukaribu au kukwepa gharama za usafirishaji. Lakini maeneo mapya ya kuzikia yapo,” anasema Sadiki.
Waliopoteza makaburi
Teddy Mmbaga mkazi wa Temeke anasema, makaburi ya ndugu zake wawili, yamepotea na eneo walipowazika, sasa wamezikwa watu wengine.
“Tunapakumbuka alizikwa hapa (anaonyesha chini ya mti) lakini sasa hivi amezikwa mtu mwingine,” anasema.
Monica Mlaponi, naye anasema amepoteza kaburi la dada yake ambaye alizikwa katika Makaburi ya Temeke mwaka 2005, lakini hivi sasa kaburi lake amezikwa mtu mwingine kabisa.
Mtembwe anasema kuwa makaburi yanayofukuliwa zaidi ni ya watoto wachanga akitaja mfano siku moja, mbili au wiki.

“Kwa vichanga wanavizika juu juu tu kisha wanafukia na wakimaliza hapo hawarudi tena na kaburi hilo huwa limesahaulika. Ndiyo maana yanafukuliwa na kutumika tena,” anasema.
Mwananchi Jumapili likiwa eneo hilo, wanaume watatu wanafika katika makaburi hayo wakiwa na maiti ya mtoto mchanga, wanachimba kaburi lisilozidi urefu wa futi nne, kisha wanakizika kichanga hicho na kuondoka.
Alama wanayoiweka ni tawi kubwa la mti ambalo limekatwa kutoka katika mti ulio karibu.
Makaburi ya Buruda
Si eneo hili tu ambalo makaburi yamekuwa yakizikiwa mara mbili au zaidi bali hata eneo la Mbagala Misheni maarufu kama Makaburi ya Buruda.
Eneo hili ambalo hata hivyo kwa sasa limefungwa kutokana na kujaa, uzikaji wake ulifanyika kwa mtindo huohuo wa kufukua la zamani na kuzikia marehemu wa sasa.
Seleman Mohamed au Keto, ambaye makazi yake yametazamana na eneo hilo anasema kabla ya kufungwa, watu walilazimisha kuzika hivyo hivyo kwa kutumia nafasi finyu waliyoiona, ambayo aghalabu huwa ni kaburi la zamani.
“Mara nyingi tu watu wamefukua mifupa hapa, lakini inakuwa siyo kazi rahisi kulifukia tena hilo kaburi bali wanaizika mifupa ile sehemu nyingine kisha wanamzika marehemu ‘mpya’,” anasema Keto.
Anasema kama taratibu za kisheria zisingefuatwa basi watu wangeendelea kuzika hapo hapo licha ya kujaa.
Mazindiko, vibaka makaburini
Mtembwe anasema katika miaka zaidi ya 30 aliyokuwa mlinzi wa Makaburi ya Temeke ameshuhudia mambo mengi ya ajabu makaburini hapo.
Anasema wapo watu ambao hufika kufanya mambo ya ajabu juu ya makaburi kutokana na imani za kishirikina.
“Wengine wanakuja kuzika vichwa vya kondoo, mbuzi au kuku. Wanafanya hivyo usiku wakati mimi sipo lakini ninajua,” anasema.
Anasema kuwa wakati mwingine anapofika eneo lake hilo la kazi, hukuta damu juu ya kaburi, nazi zilizovunjwa au mayai.
Mtembwe anaeleza kuwa baadhi yao huja mchana na humwomba kufanya matambiko katika makaburi.
“Mtu anakuja anaomba atumie kaburi la Kiislamu au la Kikristo, kuna mambo ya ajabu hapa,” anasimulia.
Si hivyo tu, bali vibaka nao wameyafanya maeneo hayo kuwa sehemu ya kujificha ili kunasa mitego yao.
Gazeti hili lilishuhudia maboksi na matambara mabovu yaliyotandikwa juu ya baadhi ya makaburi ikidhaniwa kutumiwa kwa kulaliwa na baadhi ya vibaka.
“Ni kweli wanalala juu ya makaburi, sasa kweli mtu mwenye akili timamu atalala juu ya makaburi?” anasema akihoji.
Mtembwe anasema, wanaolala juu ya makaburi usiku baadhi yao ni vibaka ambao huwavizia wapita njia usiku.
Anasisitiza kuwa wale wasiojengea makaburi watapoteza kumbukumbu ya ndugu zao na hata wakati Serikali itakapohamisha makaburi watakosa malipo.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More