ATIKA hali inayooshesha kupamba moto kwa harakati za kuteuliwa
kugombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), makundi ndani ya
chama hicho yameanza kuungana.
Mbali ya kuungana kwa makundi, pia wale wote wanaotajwa kuwania
kuteuliwa, macho na nyoyo zao vimeelekezwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho
Taifa, Rais Jakaya Kikwete, ambaye nguvu aliyonayo ndani ya vikao vya
uteuzi inatarajiwa kutumika kumpata mgombea urais.
Ingawaje viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakipinga mjadala kuhusu
mgombea urais au Rais ajaye ndani ya chama hicho kikongwe nchini, lakini
mjadala huo unatajwa kufunika hata ile mijadala muhimu kwa maendeleo ya
nchi.
Uchunguzi wa Rai umebaini kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, ameanza ‘kurudisha majeshi’, na anatajwa
kumuunga mkono Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi,
ambaye anatajwa kuwa ‘safi’, mtu asiye na kikwazo mbele ya Rais Kikwete.
“Hali
inavyoonekana sasa, Membe anaelekea kuungana na kambi ya Dk. Nchimbi,
na si yeye pekee, wale wote ambao wanampinga Lowassa lakini wanajua
hawana kura ndani ya CCM, wanaanza kumuunga mkono Nchimbi.
“Lengo
kubwa hapa ni kutengeneza mgombea mmoja mwenye nguvu kubwa ili
kumkabili Lowassa ambaye anatajwa kuwa na nguvu kubwa zaidi ndani ya
chama katika ngazi zote.
“Katika hao, yumo Waziri Samuel Sitta,
Dk. Harrison Mwakyembe na watu wao, lakini vile vile wanasahau uhusiano
mzuri na kuheshimiana kati ya Lowassa na Dk. Nchimbi.
“Pia tetesi
za kuwapo mpango wa kulikata jina la Lowassa katika ngazi ya Kamati Kuu
lisirudishwe kwenye Mkutano Mkuu ambako anadaiwa kukubalika kuliko
wagombea wengine, kunatajwa kuwa moja ya sababu za makundi kuungana,”
alisema mchambuzi mmoja wa mambo ya siasa nchini.
Mgombea
mwingine anayetajwa kupewa nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM 2015, ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira,
ambaye tofauti na wagombea wengine, yeye hana kundi wala makundi.
Kutokana
na kutokuwa na makundi, wachunguzi wa mambo wanasema haitakuwa rahisi
jina lake kukwama katika ngazi ya Kamati Kuu, hivyo uwezekano wa jina
lake kupigiwa kura na wajumbe wa Mkutano Mkuu kuchuana na wagombea
wengine ni mkubwa.
“Huyu Mzee ana advantage moja kubwa, Kanda ya
Ziwa inatajwa kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura tofauti na maeneo
mengi, na ni katika kanda hiyo hiyo Lowassa anaungwa mkono sana.
“Kama
CCM wataamua kulikata jina la Lowassa, kuna uwezekano mkubwa sana kwa
wana-CCM waliokuwa wakimuunga mkono kuhamishia kura zao kwa Wasira, na
kumchagua,” alisema mchambuzi huyo.
Wakati hali ikiwa hivyo, pia
imethibitika vigogo wa chama hicho wakiwamo wale wa kundi la
wanamtandao lililomwingiza Rais Kikwete madarakani mwaka 2005
hawaaminiani katika harakati za kugombea urais kupitia CCM.
Uchunguzi
unaonyesha vigogo wa CCM kutoka kambi zote wamekuwa wakiendesha kampeni
za chini kwa chini kwa ajili ya kujiimarisha na kisha kuweza kuteuliwa
kugombea kupitia chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.
Taarifa
zinaonyesha kwamba hata baadhi ya vigogo wanaosadikiwa kuwa kundi moja
sasa hawaaminiani jambo ambalo linaashiria kuwa vita ya urais CCM
inapamba moto siku hadi siku.
Wakati wa vikao vyake vya juu
vilivyomalizika Novemba 24 mwaka jana mjini Dodoma, CCM kilipokea na
kupitisha taarifa ya hali ya siasa ambayo kimsingi ilibainisha kuwa hali
ya siasa ndani ya chama si shwari, kutokana baadhi ya viongozi kupigana
vikumbo kuwania madaraka.
Katika taarifa hiyo, CCM kilisema chanzo kikubwa cha migawanyiko ndani ya chama hicho ni harakati za kugombea urais mwaka 2015.
Hata
hivyo, wimbi hilo la urais limeendelea kutikisa kambi ya wanamtandao
ambayo taarifa za ndani zinasema huenda suala la urais likaibua
mtafaruku mkubwa siku zijazo, hivyo kutoa mwanya kwa kundi jingine
kuibuka kidedea.
“Kuna hali ya kutoaminiana ndani ya CCM, kila
kundi sasa liko mstari wa mbele kujijega ili kuweza kujiweka kwenye
nafasi nzuri ya kutoa mgombea urais.
“Hata ndani ya kundi la
mtandao ambalo ndilo lenye nguvu kwa sasa wakubwa hawaaminiani,” alisema
mtoa habari mmoja kutoka kundi la mmoja wa kiongozi anayetajwa kutaka
kuwania urais ndani ya CCM.
Chanzo: gazeti la rai
0 maoni:
Chapisha Maoni