Jumapili, 14 Aprili 2013

Vyombo vya Habari vyashutumiwa kuchochea kesi ya Lulu


BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limevishutumu vyombo vya habari kwa kuandika habari zenye mwelekeo wa kumhukumu msanii Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu, kwamba amemuua msanii mwenzake, Steven Kanumba.

Akisoma tamko la Kamati ya Maadili ya MCT Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Jaji mstaafu Thomas Mihayo, alisema wamesikitishwa na ukiukwaji mkubwa wa maadili uliojitokeza kwa baadhi ya vyombo vya habari katika kuripoti kuhusu kifo cha msanii, marehemu Kanumba.

Alisema hatua hiyo ni ukiukwaji mkubwa uliovuka mipaka wa maadili ya uandishi wa habari.

Alisema vyombo hivyo vimemhukumu msichana Lulu kuwa amemuua msanii huyo bila kuzingatia kwamba kufanya hivyo ni kosa.

Alisema ukiukwaji huo umejitokeza baada ya msichana huyo kufikishwa mahakamani ambapo baadhi ya magazeti yanayoheshimika katika jamii yaliandika vichwa vya habari vinavyomhukumu moja kwa moja Lulu kama ni muuaji.

“Kwa mujibu wa sheria na maadili ya uandishi wa habari, mtu yeyote anayekamatwa kwa tuhuma yoyote ile ni mtuhumiwa hadi atiwe hatiani na mahakama.

“Kanuni hii ya siku nyingi katika fani ya uandishi wa habari inafahamika kwa waandishi na wahariri wote kujiepusha na habari au vichwa vya habari vinavyohukumu ambavyo vinaonekana kushawishi au kushinikiza uamuzi wa mahakama,” alisema Jaji Mihayo.

Aidha, alionya kesi ya msanii huyo si rahisi kama wengi wanavyofikiri na vyombo vya habari vifanye kazi yake kwa mujibu wa taaluma na viache kuongozwa na taarifa za pembeni, zikiwamo za katika mitandao.

Naye, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, aliwataka waandishi wa habari kuchunguza undani wa kifo cha marehemu Kanumba kwa sababu kinaingilia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.

“Nawakumbusha waandishi wenzangu, tuzame zaidi kulitazama suala hili, tukio limetokea kwa utatanishi, habari ya kifo cha Kanumba inaingilia masuala ya kijinsia, maana jamii inalishwa sumu kwamba kuna mmoja ambaye ni malaya na mwingine sivyo, hii si sawa,” alisema Kajubi.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More