Dar/Dodoma. Mvutano kuhusiana na mchakato wa
kupata Katiba Mpya unaozigonganisha Serikali na Chadema ulizidi kupamba
moto bungeni jana wakati wa mjadala wa kuhitimisha hotuba ya bajeti ya
Ofisi ya Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jana alitumia muda wake
karibu wote wa saa moja kujibu maoni na kumshambulia Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyoyatoa kuhusu hotuba ya
bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hoja za Mbowe zilizoonekana kumsumbua Pinda ni
malalamiko dhidi ya Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba, Tume ya Taifa ya
Uchaguzi na kauli yake kwamba serikalini hakuna weledi wa kuwezesha
kupanga mipango ya maendeleo.
Hata hivyo, baada ya kuhitimisha hotuba hiyo,
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisimama kuomba mwongozo wa Spika chini
ya kanuni ya 68 (7) akidai kuwa Pinda alikuwa ametoa kauli ya uongo kuwa
Chadema haikuwasilisha mapendekezo yake juu ya muundo wa Mabaraza ya
Katiba, badala yake walilalamika tu kwenye mkutano wa hadhara.
Akizungumzia, Pinda alieleza kumshangaa Mbowe kwa
kudai kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba haina weledi wakati kuna
maprofesa na kati ya hao ni Profesa Mwesiga Baregu wa Chadema.
“Hivi kweli hawa wazee na maprofesa ni mambumbumbu
kweli au ni kauli ambayo hakuipangilia. Haiwezekani kwa mjumuiko wa
wazee wote waliomo mle ndani."
“Tuwatendee haki Watanzania na tusiwakatishe tamaa
wazee wetu ambao wamezunguka nchi nzima na kufanya kazi kubwa, kama
haya ndiyo Mbowe ametumwa basi nadhani aliteleza.”
Pinda alisema kama kuna tatizo kwenye mchakato ni kutokana na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyopitishwa na Bunge.
Wakati anazungumzia suala hilo ilisikika sauti
kuwa wakati sheria hiyo inapitishwa Chadema walitoka bungeni, na Pinda
alirudia, “Nasikia kuwa mlitoka bungeni.”
Pinda alisema kutakuwa na Bunge la Katiba na
wabunge wote ni wajumbe, pia kwa Zanzibar kuna Baraza la Wawakilishi,
hivyo Mbowe kuanza kutoa maoni hayo inaonyesha wana hofu.
“Kama Chadema wana hofu basi ni jambo lingine,
nilipoisoma `speech’ (hotuba) ya Mbowe mawazo yake yanaonyesha anawaza
uchaguzi wa 2015 na si kitu kingine,” alisema Pinda na kupigiwa makofi
na wabunge wa CCM.
Alisema Mbowe alimtisha zaidi pale aliposema kuwa wataitisha maandamano nchi nzima kupinga suala hilo, kitu ambacho si sawa.CHANZO: Mwananchi
0 maoni:
Chapisha Maoni