Uamuzi huo ni nafuu kwa baadhi ya waliokuwa
wagombea walioenguliwa na kupinga uamuzi huo kwenye uchaguzi uliojaa
utata kiasi hata cha baadhi ya wagombea kukimbilia mahakamani
wakiishtaki TFF, wakipinga kuenguliwa kwao.
Kabla hata ujumbe wa Fifa kutua nchini mwanzo wa
mwezi uliopita kusuluhisha mgogoro huo mkubwa ndani ya TFF, Serikali kwa
upande wake ilikwishaingilia kati na kuusimamisha uchaguzi huo, ikitaka
kwanza kufanywa marekebisho kadhaa ya kikatiba ndipo uchaguzi huo
ufanyike.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema jana jijini
Dar es Salaam kuwa, Fifa imebaini upungufu siyo tu namna mchakato wa
uchaguzi ulivyoendeshwa, bali pia udhaifu wa vipengele kwenye katiba na
kuagiza kufanywa marekebisho haraka.
Tenga alisema, Fifa wanataka kuona marekebisho
yanafanywa mapema kabla ya kuanza upya mchakato wa uchaguzi, ambao agizo
pia linaelekeza ufanyike kabla ya Oktoba 13.
“Kamati ya Utendaji TFF itakutana Mei 9 kwa lengo
la kutoa taarifa za kuanza mchakato wa marekebisho ya katiba kama Fifa
walivyoagiza katika taarifa yao kwetu,” alisema Tenga.
“Niseme tu kwamba, mchakato wa kwanza wa uchaguzi
ni batili, zoezi hili linaanza upya, tena haraka iwezekanavyo. Haya ni
maagizo ya Fifa,” aliongeza Tenga.
Akifafanua zaidi Tenga alisema: “Tunatakiwa kwanza
kuunda kamati mbili, maadili kwa ngazi ya mwanzo na ngazi ya rufaa.
Kamati hizi zitakuwa na kazi ya kushughulikia matatizo yote ya kimaadili
kwa wale wote watakaokwenda kinyume na matakwa ya katiba ambayo pia
Fifa imeagiza ifanyiwe marekebisho.” Aliongeza: “Kamati hizi zitasaidia
kuhakikisha haki inatendeka na kuondoa migogoro kama tulivyoona awali.”
Kiini cha mgogoro huo kilikuwa ni kuenguliwa kwa
wagombea wa nafasi ya makamu wa Rais, Michael Wambura na Jamal Malinzi
aliyeomba urais. Wagombea hao walitua Fifa wakilalamikia kuenguliwa
kwao.
Kuenguliwa kwao na wengine kadhaa kulichafua hali
ya hewa, huku wadau wengi wakiitupia lawama TFF kupitia kamati zake za
uchaguzi na rufaa kwa madai ya kuwapo na upendeleo wa kuwabeba baadhi ya
wagombea waliodaiwa kuwa na masilahi nao.
Ujumbe wa Fifa ulikuwa nchini na kukaa siku tatu
ukiwahoji baadhi ya wagombea na viongozi wa TFF na kisha kukutana na
serikali na kuahidi kutoa jibu baada ya wiki moja.
0 maoni:
Chapisha Maoni