Ijumaa, 3 Mei 2013

Serikali kukaza uzi timuatimua wanafunzi wakorofi vyuo vikuu

Dodoma. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesisitiza kuwa itaendeleza utaratibu wa kuwafukuza wanafunzi wa vyuo vikuu ambao watakuwa na tabia za utovu wa nidhamu na migomo isiyokuwa na lazima.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo.
Alisema Serikali haina kigugumizi cha kuona ni kwa nini isiwafukuze wanafunzi wa aina hiyo ambao wanakuwa ni kichocheo cha migogoro.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), ambaye alitaka kujua mkakati wa Serikali kuwarudisha wanafunzi wa vyuo vikuu ambao walifukuzwa masomo yao
kutokana na migogoro iliyoibuliwa vyuoni mwao.
Katika swali la msingi Mnyika alitaka kujua hatua za Serikali katika kuwarudisha wanafunzi hao kutoka vyuo vya Dodoma (Udom), Dar es Salaam na Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi (MUHAS).
Mbali na hilo, aliomba ripoti ya Tume ya Rais iliyoundwa mwaka 2011 kwa ajili ya kuangalia migogoro hiyo kwa wanafunzi ambayo imedumu kwa muda mrefu ili ipelekwe bungeni na kujadiliwa kabla ya kumshauri Rais jambo la kufanya.
Naibu Waziri alisema katika migogoro hiyo, kuna maeneo ambayo wanafunzi walisimamishwa masomo na baadhi walirudishwa masomoni, lakini wengine bado hawajarudishwa.
“Mfano, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanafunzi waliosimamishwa ni 99, lakini 78 walirudishwa na 21 hawajarudishwa, kwa Udom walisimamishwa 570 lakini 563 walirudishwa masomoni na 7 wamefukuzwa kabisa, kingine ni MUHAS ambapo walisimamishwa wanafunzi 115 wengine wamerudi na wengine watarudi Desemba mwaka huu wakati wanafunzi wawili wamefukuzwa kabisa,” alisema Mulugo.
Kuhusu ripoti ya Rais, Mulugo alisema ilikuwa ni tume maalumu kwa ajili ya kumsaidia Rais, hivyo siyo lazima ripoti yake kupelekwa bungeni kama ambavyo wabunge wanataka.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More