WADAI ANA UWEZO MDOGO WA KUONGOZA
MWENYEKITI wa taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim
Lipumba, amesema Spika wa Bunge, Anna Makinda, ameshindwa kukiongoza
chombo hicho kwa maslahi ya taifa, badala yake amegeuka kuwa kinara wa
upendeleo kwa chama na serikali ya CCM.
Profesa Lipumba amemtaka Makinda atafakari na apime uwezo wake wa
kiuongozi katika Bunge na afanye maamuzi magumu ya kubadilika kifikra
kwa kuacha upendeleo anaoufanya kwa sasa.
Kauli hiyo aliitoa juzi jijini Mwanza alipokuwa akizungumza na Tanzania
Daima, muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa kujadili na
kuchangia mawazo juu ya maendeleo kwa wote mkoa wa Mwanza, uliofanyika
katika Hoteli ya JB Belmont.
Alisema Spika amejionyesha uwezo wake mdogo wa kuongoza Bunge na akubali
kushauriwa au kubadilika kifikra ili alinusuru Bunge lisiendelee
kudharaulika ndani na nje ya nchi.
“Spika ameshindwa kutenda haki kwa nafasi yake aliyonayo bungeni.
Hawatendei haki wabunge wa vyama vya upinzani….mbaya zaidi kiti chake
kimeonesha wazi kuegemea chama na serikali ya CCM katika mijadala ya
kitaifa na wananchi wake.
Profesa Lipumba alitaka Katiba mpya ijayo lazima itamke Spika asitokane
na wabunge, bali atoke nje ya Bunge ili kukiongoza chombo hicho kwa
manufaa ya taifa zima.
Alisema Bunge ni chombo muhimu sana katika maendeleo na kugawa haki kwa
wote, hivyo kinapoongozwa na mtu anayeegemea upande wa serikali na chama
chake anawanyima Watanzania kupata haki za kimaendeleo.
“Tunataka Katiba mpya izuie Spika asitokane na wabunge. Tunataka Spika
atoke nje ya Bunge ili aweze kutenda haki kwa Watanzania wote,” alisema.
Alisema uwajibikaji mbovu wa Bunge unazorotesha sana kasi na mwelekeo wa
maendeleo ya wananchi na taifa zima na kwamba upo ulazima Watanzania
kufanya maamuzi magumu ya kuiondoa madarakani CCM ifikapo mwaka 2015.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, serikali ya CCM imeshindwa kutekeleza
matakwa ya wananchi waliyoiweka madarakani, hivyo hawana budi kuiangusha
CCM katika uchaguzi mkuu ujao ili wapate maendeleo.
Wakati huohuo, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, amewashambulia
watumishi wa Bunge kwa kusema karibu nusu ya watumishi hao ni mzigo
kutokana na kushindwa kufanya kazi katika kiwango kinachotakiwa.
Ndugai aliitoa kauli hiyo mjini hapa jana alipochangia katika semina ya
wabunge iliyoandaliwa na tume ya mipango iliyojadili jinsi ya
uendelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema kumekuwepo na tatizo la viongozi kufanya uozo ndani ya ofisi
zao, lakini cha kushangaza hakuna mtu mwenye ujasiri wa kuwafukuza na
matokeo yake watumishi wanaendelea kufanya jambo ambalo si sahihi.
“Mfano mzuri kuna walimu wanafelisha wanafunzi wao karibu kwa miaka
mitano mfululizo, lakini hakuna mtu anayewafukuza au kuwapa adhabu
yoyote jambo hilo ni hatari na kuendeleza kufanya kazi kwa mazoea.
“Sisi wabunge ambao tuko majimboni tunapata shida sana na watumishi wa
halmashauri wengi wanafanya kazi hovyo, lakini pia hata bungeni si wote
ambao wanafanya kazi kwa uaminifu, hata hapa karibu nusu ya wafanyakazi
wa Bunge ni mzigo lakini hakuna mtu ambaye anaweza kuwawajibisha,”
alisema Ndudai.
Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida (CCM), akichangia alisema kuwa
bado kuna tatizo kubwa la watumishi wa serikali kulindana na ndiyo maana
kuna uharibifu.
Lulida alisema kinachosumbua katika mipango mingi serikalini ni kuwepo
kwa urasimu, upendeleo ikiwa ni pamoja na kulindana pasipo na sababu za
msingi.
Akichangia hoja hiyo, mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, alisema kamwe
Tanzania haiwezi kuwa na maendeleo kutokana na kuwepo kwa utamaduni wa
kufanya kazi kwa mazoea.
Pia alisema mawaziri hawawezi kufanya vizuri katika kuendeleza miradi
kwa kuwa wanakwamishwa na makatibu wakuu wa wizara husika kwa
kuwachukulia mawaziri kama wapitaji na wao ndio wa kudumu.
“Tumekuwa tukililia mfumko wa bei nani asiyejua kuwa wafanyabiashara
wanafanya makusudi kuficha bidhaa, ili waweze kupata nafasi ya
kupandisha bei bidhaa hizo? Fikiria vipo viwanda vya kuzalisha sukari
lakini wenye viwanda wanafanya kusudi kuzalisha kidogo.
“Waziri Mkuu amepiga kelele juu ya kupanda kwa bei ya sukari lakini
hakuna kilichofanyika, jambo ambalo ni hatari na kamwe hakuna maendeleo
ambayo yanaweza kujitokeza kama hali hiyo itaendelea katika maeneo
mbalimbali,” alisema Lugola.
0 maoni:
Chapisha Maoni