NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai, jana alilazimika kuliahirisha Bunge mara mbili na kusitisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa baada ya wabunge wa CUF kumchachamalia mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje (CHADEMA).
Hatua hiyo ilikuja wakati Wenje akiwasilisha hotuba ya kambi ya upinzani na kutaja vyama vya siasa vya nje rafiki vinavyoshirikiana na vyama vya CCM, CHADEMA na CUF, akisema msimamo wa kiliberali wanaoufuata CUF unashabikia ushoga na usagaji.
Pamoja na Wenje kutokuwa ameufikia ukurasa wa nane uliokuwa na maneno hayo, hotuba yake ilikatizwa kwa mwongozo ulioombwa na mbunge wa Mtambile, Masoud Abdallah Salim (CUF).
Salim alitumia kanuni ya 68 (1) sambamba na 64 (1) (a) (c) akisema maneno yaliyotumika yanaudhi, kizandiki, kihuni, kishenzi, kifedhuri kisha akamtaka Wenje ayafute na kuwaomba radhi.
“Anasema kuwa chama cha CUF, kutokana na itikadi yake ya mrengo wa kiliberali ambayo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na kupigania haki za ndoa ya jinsia moja, usagaji na ushoga.
“Kwamba hii ni kwa mujibu wa tangazo lao kwenye mtandao wao wa umoja wa maliberali ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa Haki na Usawa wa Uingereza, Lynn Featherstone, kutoka chama cha Liberal Democrats wakati chama hicho kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu ndoa za jinsia moja kama haki ya mtu mmoja mmoja,” alisema.
Salim aliitaka CHADEMA ifute maneno hayo na kisha kuomba radhi, vile vile Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge iwachukulie hatua, vinginevyo CUF walitishia kuchukua hatua.
Wakati Salim akiomba mwongonzo huo, wabunge wa CUF na CCM walikuwa wakichagiza kwa maneno ya chini kwa chini wakisema…wamezoea hao, wapigwe, waondoe maneno, washenzi…wakome kabisa.
Baada ya mbunge huyo kumaliza, Naibu Spika, Job Ndugai, alimuuliza Wenje kama ana lolote la kusema na ndipo akaomba wabunge wenzake wamsikilize na kujaribu kuelewa alikuwa akimaanisha nini.
“Kwa heshima kubwa naomba wabunge wanielewe, hapa tumeeleza vyama vya nje vyenye mahusiano na vyama vya hapa ndani, nilieleza CCM ilivyo na mahusiano na vyama vya kikomunisti, CHADEMA inahusiana na vyama vya kidemokrasia na CUF inahusiana na vyama vya kiliberali, hapa tunazungumzia itikadi,” alisema Wenje.
Hata hivyo, hotuba yake ilikatizwa na wabunge wa CUF waliokuwa wakiongozwa na Salim, wakisimama na kuanza kuporomosha maneno mazito wakisisitiza hotuba hiyo haisomwi, huku wengine wakichana vitabu vya hotuba hiyo.
Ndugai baada ya kuona hali hiyo, ambapo baadhi ya wabunge hao wakiwemo wa CCM walikuwa wakichochea wakitaka Wenje apigwe alitangaza kuliahirisha Bunge kwa muda hadi saa 11 jioni na kuomba Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ikutane.
Licha ya Bunge kuahirishwa, mzozo uliendelea ndani ya ukumbi wa Bunge kwa wabunge wa CUF kutaka kumpiga Wenje.
Wakati vurugu hizo zikiendelea wabunge wengi wa CHADEMA hawakuwemo ukumbini maana walikuwa kwenye kikao na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, kwenye ofisi za kambi, jambo lililowafanya askari wa Bunge kusogea karibu na Wenje.
Bunge laahirishwa tena
Baada ya mapumziko ya mchana Bunge lilianza kwa Ndugai kumwita Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Maadili, John Chiligati, kueleza uamuzi uliofikiwa.
Chiligati alisema kuwa walikutana na Salim kama mlalamikaji ambaye msimamo wake ulikuwa ni kumtaka Wenje aombe radhi na kuondoa maneno hayo, masharti ambayo Wenje alikubaliana na moja la kuondoa maneno.
“Lakini aliiahidi kamati kuwa anakwenda kuibadili hotuba yake kwa kuondoa maneno hayo lakini hakuna mabadiliko aliyofanya maana maneno aliyoweka kwa Kingereza ni yaleyale aliyotakiwa kuondoa,” alisema.
Hata hivyo, Wenje alipopewa muda aseme kama anakubaliana na ushauri huo, alitoa ufafanuzi huku akionyesha nyaraka za makubaliano ya vyama vya kiliberali yaliyofikiwa mwaka 1997 na CUF kikiwa mshiriki, kisha akakataa kuomba radhi kwa maelezo kuwa haoni kosa.
Kutokana na msimamo huo, Ndugai alimwamuru Wenje kuomba radhi na kuondoa maneno hayo ndipo aweze kuendelea na hotuba yake, lakini mbunge huyo aligoma katakata kuomba radhi na hivyo akatakiwa kuketi.
“Suala hili nalirudisha kwenye kamati ya maadili ili itushauri zaidi na kwa hali hiyo siwezi kuendelea, nasitisha Bunge hadi kesho saa tatu asubuhi na tutaendelea na Wizara inayofuata ya Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo,” alisema Ndugai.
Wabunge welionekana kubishana kwenye makundi nje ya ukumbi huku wengi wa CCM na CHADEMA wakimsifu Wenje na kumlaumu Ndugai kuwa alishindwa kulimudu Bunge.
Mapema asubuhi
Vugugu hizo zilihamia nje ya Bunge ambapo wabunge wa CUF walikuwa wakimfuata Wenje ili kumshambulia lakini wabunge wenzake wa CHADEMA na CCM walimsihi asifanye malumbano na hivyo kumsindikiza hadi ofisi za kambi hiyo wakiongozwa na Livingstone Lusinde.
Wabunge wa CUF walikuwa wakiporomosha maneno makali na matusi dhidi ya Wenje na viongozi wengine wa CHADEMA wakiapa kuwa liwalo na liwe lakini hotuba hiyo haitasomwa hadi maneno hayo yaondolewe.
Baadhi yao, Khatib Haji (Konde), Bungala (Kilwa Kusini), Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe), Rukia Kimwaga (Viti Maalum), Salim (Mtambile) na wengineo walikuwa wakiporomosha matusi mazito wakidai kuwa CHADEMA inawadhalilisha wakati chama chao kimekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ushoga.
Hata hivyo, mabishano hayo yaliibua pande mbili ambapo baadhi ya wabunge wengi wa CCM walikuwa wakiwaunga mkono CUF wakati wengine walikuwa wakipinga na kusema kuwa hawakufasiri vyema maneno ya Wenje.
“Wacha iwapate maana wakati tulipolalamikia hotuba za CHADEMA kuwa na maneno ya kuudhi dhidi ya CCM walikaa kimya, sasa kwa nini nao wasingekuwa wavumilivu hadi amalize hotuba yake. Kwanza ukurasa wenyewe alikuwa hajaufikia pengine angeruka,” alisema mbunge wa CCM.
Naye Ndugai, aliwarushia lawama waandishi wa habari akidai kuwa wanaibeba CHADEMA hata pale wabunge wake wanapofanya mambo ya hovyo.
“Hawa wanakwenda kuwa watawala, sasa kwa mwendo huu unadhani itakuwaje lakini nyie waandishi ndio mnawabeba. Hizi hotuba tunajua sio za kambi wanaandika wenyewe,”
Hata hivyo Ndugai alikwepa kufafanua ni kwa nini kiti cha Spika hakizipitii mapema kabla ya kusomwa bungeni.
0 maoni:
Chapisha Maoni