Habari zinasema tayari Jalada la mashitaka yao limefikishwa mikononi kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa uamuzi wa sheria.
Watu watatu wamekwisha kufa kutokana na mlipuko huo huku majeruhi wakiwa 66. Baadhi yao walikimbizwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas jana alitaja majina ya watuhumiwa wanaoshikiliwa na jeshi hilo kwa mahojiano.
Watuhumiwa hao ni Victor Ambrose Kalisti (20), mkazi wa KwaMrombo Arusha ambaye ni dereva wa pikipiki (Boda boda).
Wengine ni Joseph Yusuph Lomayani (18) ambaye pua ni dereva wa pikipiki mkazi wa KwaMrombo Arusha.
Kamanda aliwataja watuhumiwa wengine kuwa ni Mohamed Suleiman Said (38) wa Ilala Dar es Salaam.
Mtuhumiwa Said ndiye anayedaiwa kuwa mwenyeji wa watuhumiwa wengine na alitumika piakuwachukulia vyumba katika Hoteli ya Aquline jijini Arusha, alisema Sabas.
Wengine ni George Bathoromeo Silayo (23) mfanyabishara mkazi wa Olasiti, Said Abdallah Said (28,) raia wa Falme za Kiarabu (Abu Dhabi).
Aliwataja wengine kuwa ni Abdulaziz Mubarak (30) kutoka Saudi Arabia, Jassini Mbarak (29) wa Bondeni Arusha, Foud Saleem Ahmed (28) na Said Mohsen, wote kutoka Falme za Kiarabu.
Tukio la kurushwa kwa bomu hilo lilitokea Mei 5 mwaka huu, saa 4.30 kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti.
Ibada maalumu ya uzinduzi wa Parokia hiyo ilikuwa ikiendeshwa na Balozi wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Francisco Padilla akisaidiana na mwenyeji wake, Askofu wa Jimbo Kuu la Arusha Joseph Lebulu.
“Wakati mgeni rasmi akijiandaa kukata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi, ghafla mtu aliyekuwa amejificha pembeni ya choo jirani, upande wa Kaskazini, alirusha kitu kizito mbele ya waumini waliokuwa nje ya kanisa.
“Kitu hicho kilirushwa umbali wa mita 20 kikiwa na ukubwa wa ngumi ya mtu mzima. Kilielekea kwenye mkusanyiko wa waumini na kudondoka chini na kulipuka mithiri ya bomu,”alisema.
Alisema muundo wa bomu hilo hauonyeshi kama lilitengezwa kienyeji bali lilitengezwa kwa utaalamu.
Mpaka sasa watuhumiwa ambao ni raia wa kigeni wameonyesha ushirikiano wa kudai kwamba walikuwa nchini kushiriki harusi, alisema.
Hata hivyo, alisisitiza kwamba watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa.
0 maoni:
Chapisha Maoni