Jumatano, 1 Mei 2013

Mei Mosi: Wafanyakazi walia na kodi

 Wakati leo Watanzania wakiungana na wenzao duniani kusherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi), wadau wa sekta mbalimbali nchini wameitaka Serikali iwapunguzie kiwango cha kodi wanachokatwa (Paye).
Kwa kipindi kirefu sasa, wafanyakazi nchini wamekuwa wakilalamikia kodi kubwa inayotozwa kwenye mishahara na kiwango kidogo cha mshahara wenyewe. Kwa sasa kima cha chini cha mshahara ni Sh180,000 kwa mwezi.

Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), limeitaka Serikali kupunguza makato makubwa ya kodi na mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia wafanyakazi kupata kiasi kidogo cha fedha katika mishahara yao na kuishi katika mazingira magumu.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicolaus Mgaya alisema jana kuwa madai hayo ni ya muda mrefu, lakini hayajawahi kufanyiwa kazi, jambo ambalo limewafanya wafanyakazi wengi kukosa matumaini.
Alisema, awali walitoa mapendekezo ya kima cha chini cha mshahara kuwa Sh315,000 lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika na badala yake wamekuwa wakiongezewa kiasi kidogo kisichokidhi mahitaji.Mgaya alisema nyongeza ya mishahara imekuwa ndogo wakati makato ya kodi ni makubwa.
“Bado tunaendelea na malalamiko yetu ya nyongeza ya mishahara na kupunguzwa kwa makato ya kodi kwa sababu Serikali imeshindwa kutekeleza. Tutayawasilisha tena kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kesho (leo),” alisema Mgaya.

Alisema nauli zimepanda, lakini wafanyakazi bado wanalipwa mishahara duni, jambo ambalo linawafanya waendelee kuishi kwenye mazingira duni. Mbali na nauli, pia kuna tatizo la kupanda kwa mahitaji ya muhimu kama vyakula na malipo ya huduma za umeme na maji.
Hata hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally amevitaka vyama vya wafanyakazi nchini kupambana na mfumo badala ya kudai nyongeza ya mishahara pekee.
“Tanzania kuna mfumo wa unyonyaji, ili kuuondoa, vyama vya wafanyakazi vinatakiwa kuungana pamoja na kuwaunganisha wavuja jasho wengine kama mamalishe, madereva wa mabasi na wengineo ili wadai mfumo wa haki,” alisema Bashiru na kuongeza:

“Mfumo wetu ni wa kuwaongezea walionacho na kuwapunja wasionacho, wanatakiwa kuwa na mapambano ya muda mrefu ambayo yatawakomboa moja kwa moja, waige vyama vya wafanyakazi vya nchi jirani.”

Alisema hata kama mishahara itaongezwa, haitaweza kuwasaidia kwa sababu ya mfumo mbovu wa sasa uliokosa usimamizi ambao unashindwa kuzuia kupanda kwa gharama nyingine za maisha na hivyo kufanya kila jambo zuri kugeuka msiba kwa Watanzania.
Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Profesa Gaudance Mpangala alisema tatizo lipo katika mfumo wa uchumi, kwamba pato la Taifa lipo kwa ajili ya watu fulani na si kwa Watanzania wote... “Mfumo wetu ni wa ubepari uchwara na bado unatawaliwa na mabepari. Hata mawazo ya kutawala uchumi wetu yanatoka nje, hapa kwetu tuna tatizo kubwa tumeushindwa ubepari.”
Alisema ili kujinusuru, wafanyakazi wanatakiwa kudai masilahi yao kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha pengo kati ya wenye nacho na wasio nacho linapungua.
“Ufisadi umekuwa kikwazo karibu katika kila sekta, nadhani haya ndiyo mambo ya kupambana nayo na mapambano hayo yatafanikiwa iwapo wafanyakazi watakuwa kitu kimoja,” alisema Profesa Mpangala.
Mhadhiri Mwandamizi wa UDSM, Dk Frank Tily alisema kikwazo kikubwa kwa wafanyakazi nchini kinatokana na uongozi kushindwa kusimamia mambo muhimu hasa uchumi.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema hatma ya wafanyakazi ipo mikononi mwao wenyewe na kuwataka kuchukua hatua kama Serikali imeshindwa kutekeleza madai yao.
“Mwaka 2010 wafanyakazi walifanya sherehe zao wao wenyewe bila kuihusisha Serikali kwa sababu ya ahadi hewa, mwaka 2011 na mwaka jana Serikali imetoa ahadi nyingi kwa wafanyakazi, imetekeleza? Wafanyakazi wanatakiwa kuanzia hapo,” alisema.
Nacho Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimesema tambo za Serikali kwamba imepiga hatua kiuchumi hazisaidii kwa kuwa maendeleo hayo yameshindwa kusaidia kuondoa umaskini na kuzalisha ajira mpya kama inavyoelezwa.
Katika ripoti yake ya Haki za Binadamu ya mwaka 2012 iliyotolewa jana, kituo hicho kimesema kati ya watu milioni 24 wanaochangia nguvukazi ya taifa, asilimia 8.8 hawajaajiriwa huku wengi wao wakiwa ni vijana wa umri wa kati ya miaka 15-24.
Ripoti hiyo imesema idadi kubwa ya Watanzania, wasomi na wasiosoma hawana kazi, huku wengi wao wakihangaika kupambana na changamoto za kuhama vijijini kwenda mijini kutafuta kazi.
Imeandikwa na Fidelis Butahe, Patricia Kimelemeta na Goodluck Eliona
CHANZO: mwanachi

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More