Jumapili, 5 Mei 2013

Moto wamwakia Dk Kawambwa


Dar/Dodoma. Siku moja baada ya Serikali kuchukua uamuzi mgumu wa kuyafuta matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 na kuamua yaandaliwe upya, wasomi, wanaharakati, wanasiasa na wanasheria wameitupia lawama Serikali wakitaka wote waliosababisha uzembe huo kushtakiwa kwa kusababisha vifo na udhalilishaji.
Juzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera (Uratibu na Bunge), William Lukuvi, wakati akitoa kauli ya Serikali bungeni kuhusu taarifa ya awali ya Tume ya Taifa ya Kuchunguza Matokeo ya Kidato cha Nne alisema kuwa, wameagiza Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kuweka viwango ili matokeo ya wanafunzi yalingane na juhudi zao.
Uamuzi huo wa Serikali umetokana na matokeo mabaya ya mitihani ya mwaka jana, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya wanafunzi walipata alama sifuri.
Wakizungumza na Mwananchi Jumapili kwa nyakati tofauti jana, wadau hao walisema kuwa licha ya wahusika kujiuzulu wanatakiwa pia kushtakiwa kutokana na uzembe wa makusudi.
Mbunge wa Kuteuliwa, James Mbatia alisema kuwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa anatakiwa kufukuzwa kazi na kushtakiwa kutokana na matokeo hayo mabaya.
Alisema haitoshi Dk Kawambwa kujiuzulu au kufukuzwa kazi, bali pia anatakiwa kushtakiwa kwa matokeo hayo, yaliyosababisha pia mauaji ya wanafunzi wanne, aliyosema hayakutokea kwa bahati mbaya, bali ni mpango maalumu ulioandaliwa na watendaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
“Kwa maneno aliyoyatoa, Waziri (Dk Kawambwa) wakati wa kukataa hoja yangu, haitoshi kujiuzulu tu, angekuwa anajificha asionekane hadharani kwa sababu ni aibu,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Kuna watu wanatakiwa washtakiwe kwa kusababisha maafa haya. Matokeo haya hayakutokea kwa bahati mbaya yaliandaliwa kwa makusudi, ni wauaji hawa!”
Aliionya Serikali kutochezea akili za Watanzania na kwamba familia za waliopoteza maisha kwa matokeo hayo zipewe kifuta jacho.
Mbatia aliongeza kuwa, taarifa alizonazo ni kwamba kutokana na matokeo hayo mabaya ya mtihani, baadhi ya wasichana wamekata tamaa na kuolewa.
Februari mwaka huu, mbunge huyo aliwasilisha hoja binafsi bungeni, akitaka kuundwa kamati teule kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya elimu nchini akieleza sababu kuwa hakuna mitalaa tangu Tanzania ipate uhuru na ipitie sera za elimu nchini. Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na Serikali ikidai kuwa kuna mitalaa inayokidhi viwango.
Alisema wanafunzi wanafahamishwa shuleni kuwa daraja D ni kuanzia alama 21 hadi 40; C kuanzia alama 41 hadi 60; B kuanzia 61 hadi 80 na A kuanzia 81 hadi 100, lakini Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) lilibadili mfumo huo bila waraka wowote.
Kauli ya LHRC
Mwanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hamis Mayombo alisema ndugu wa vijana waliojiua kutokana na matokeo mabaya ya mtihani huo wa kidato cha nne, wanaweza kwenda mahakamani kufungua kesi ya madai kutokana na uzembe uliojitokeza.
“Kisheria kesi inayofunguliwa hapa ni ya madhara na ikithibitika kuwa Serikali ilisababisha madhara hayo ya kifo, wanafungua kesi hiyo ili kulipwa fidia,” alisema Mayombo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo hicho, Dk Helen Kijo-Bisimba alisema kutokana na matokeo hayo kuna baadhi walipoteza maisha kwa kujiua, walipigwa na wazazi au walezi, ndugu zao na wengine walidhalilishwa vya kutosha.
“Kabla ya kutangazwa kwa matokeo hayo walitakiwa kuyaangalia kwa umakini kama yako fasaha, lakini kwa hili limepoteza uaminifu kwa wananchi” alisema Dk Bisimba na kuongeza:
“Itakuaje hao waliokwishajiua yakirudiwa tena wakakutwa wamefaulu? Inatia shaka mfumo wetu wa elimu na inawezekana hata matokeo ya nyuma yawezekana yalikosewa kwa uzembe wa watu ambao umefika wakati wa kuwajibishwa na kuchukuliwa hatua stahiki”.
Waziri afafanua
Waziri wa Elimu Dk Shukuru Kawambwa hakupatikana alipotafutwa jana lakini Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alipotafutwa kueleza endapo uamuzi huo wa Serikali unaweza kumfanya kuwajibika kwa kujiuzulu hakuwa tayari kueleza, badala yake alitoa ufafanuzi juu ya tamko hilo alilotoa Waziri Lukuvi.
“Waziri Lukuvi alitoa taarifa ya awali tu kwani tume bado inaendelea na kazi yake. Kuna masuala ya vitabu, uwajibikaji, ushirikiano kati ya Wizara ya Elimu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi).
Hata hoja ya Mbatia, zote hizi tume itakapokamilisha kazi yake itaeleza hatua ya kuchukua,”alisema Mulugo na kuongeza:
“Kuna mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi kwa haraka kwa muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu na taarifa hiyo ni matokeo ya utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Mawaziri kuhusu kurudiwa kuandaliwa kwa matokeo hayo.”
Wasomi wanena
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Morogoro, Dk George Shumbusho alisema kuwa kurudiwa kuandaliwa kwa matokeo hayo ni mkanganyiko na kwamba kilichotakiwa ni wanafunzi kufanya mtihani upya.
“Kutatokea matatizo na malalamiko kwa uamuzi huu. Kama mimi, ningetunga mtihani mwingine na wanafunzi wakaandaliwa kwa ajili ya kufanya huo mtihani,” alisema na Kuongeza:
“Matatizo yaliyojitokeza hayawezi kutatuliwa kwa kurudiwa kuandaliwa bali ni kufanya mtihani upya na kusahihishwa upya, hapo ndipo hapatakuwapo na malalamiko”alisema.
Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Profesa Gaundence Mpangala alisema kufeli kwa wanafunzi hakukuanza mwaka jana ni mfululizo wa matokeo mabaya tangu mwaka 2010 hadi 2012.
Alisema watendaji wa Necta wameandaa mtindo mpya wa uandaaji wa matokeo bila kuwashirikisha wahusika ni jambo la hatari na kwamba kinachotakiwa siyo kurudia mitihani bali kuangaliwa tatizo lenyewe linalosababisha kushuka kwa kiwango cha ufaulu kila mwaka.
“Walimu wakipewa motisha ya kutosha, vifaa vya kufundishia vikiwepo, walimu wenye sifa nafikiri hili ndilo litakuwa suluhisho la kudumu na si hivi ilivyo,” alisema Profesa Mpangala na kuongeza:
“Serikali ingechukua programu ya dharura ya kuandaa walimu na kuhakikisha vifaa vyote vya kufundishia na kumaliza matatizo ya walimu na hili la kurudia kuyaandaa matokeo lingekuwa jambo linalofuata”.
Profesa Mpangala ambaye alifanya kazi kwa zaidi ya miaka mingi katika Baraza hilo hadi miaka 1981, alisema kuwa kurudiwa kuandaliwa kwa matokeo hayo kunaweza kuhalalisha ubovu zaidi.
Sababu za matokeo mabaya
Waziri Lukuvi alisema ufaulu umeshuka zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya mchakato wa kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani mwaka 2012, mfumo uliotumika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti na ule uliotumika miaka iliyotangulia.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More