Jumatatu, 27 Mei 2013

Chadema yaipunguza kasi CCM Tabora

*Viongozi CCM wazomewa katika mkutano wa hadhara
*Ni baada ya kuanza kuwatukana viongozi wa Chadema

Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage













VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Tabora, juzi walijikuta katika wakati mgumu, baada ya kuzomewa na wananchi kwenye mkutano wa hadhara. Tukio hilo la aina yake lilitokea wakati viongozi wa chama hicho ngazi ya mkoa, akiwemo Mbunge wa Tabora Mjini, Aden Rage, walipokwenda kuhutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Stendi ya mabasi ya zamani mjini hapa.

Mkutano huo wa hadhara ulifanyika siku chache baada ya ule wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, ambaye aliwaeleza wananchi, kuwa wabunge wa CCM mkoani Tabora hawawakilishi vema wapigakura wao na kwamba kutokana na hali hiyo, wabunge wa Chadema wameamua kupigania haki zao.
Baada ya Zitto kuhutubia katika uwanja huo, viongozi wa CCM waliamua kujibu mapigo wakiongozwa na Rage ambapo juzi waliamua kuitisha mkutano huo.

Dalili za CCM kuzomewa katika mkutano huo, zilianza mapema kabla ya kuanza kwa mkutano kwani baadhi ya wananchi walisikika wakikejeli kwamba wanataka kusikia sera si majigambo, matusi wala blaa blaa nyingine.

“Tunataka barabara za lami kuanzia Tabora-Nzega, Tabora-Urambo na ile ya Itigi-Tabora, vinginevyo wapisheni peoples power,” walisikika baadhi ya wananchi wakisema.

Wakati hayo yakitokea, Katibu wa CCM, Mkoa wa Tabora, Idd Ame, alianza kuhutubia huku akikiponda Chadema jambo ambalo liliwakera wananchi na kuanza kumzomea.

“Ndugu zangu wananchi, hebu angalieni mnavyodanganywa, hivi hawa Chadema wanajigamba kujenga barabara wakati wao siyo watoaji wa fedha, Serikali ya CCM ndiyo yenye dhamana ya fedha wala siyo hao wanafiki na waongo wakubwa.

“Mtu anaacha jimbo lake huko Kigoma anakuja hapa Tabora kuwafundisha siasa chafu, huu ni ‘upumbavu’ hatuwezi kuuvumilia,” alisema Ame.

Baada ya kauli hiyo, mkutano ulivurugika na wananchi walianza kuzomea kwa maneno ya kejeli wakidai wanataka sera na siyo matusi, huku wengine wakisema CCM ni wepesi wa kujibu hoja za Chadema na siyo kuanzisha hoja zao wenyewe.

Aidha, katibu huyo aliendelea kuwaambia wananchi kuwa kama wataendelea na tabia ya kuwasikiliza Chadema, watasababisha mapigano bila kutarajia.

“Hapa tuko kamili, endeleeni kuzomea tu, tutaumizana kweli kweli, hapa msifikiri hatuwezi na tutawashitaki viongozi wa Chadema Tabora kwa kutufanyia fujo kwenye mkutano wetu,” alisikika akisema Ame.

Wakati akisema maneno hayo, yaliyoonekana kutowafurahisha baadhi ya viongozi wa meza kuu ambapo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), John Mchele, aliamua kwenda kumnong’oneza katibu huyo ili aache malumbano na wananchi.

Huku mkutano huo ukikosa utulivu, fujo kubwa zilizuka baada ya vijana wa ulinzi wa CCM wanaojulikana kama ‘Green Guard’ kuamua kutuliza vurugu hizo.

Baada ya vurugu kutulia kidogo, Rage alipanda jukwaani kuhutubia na baadaye alitoa Sh milioni 68 kwa kata kumi za Manispaa ya Tabora, ambapo kila kata ilikabidhiwa hundi yake kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa vyoo, umaliziaji nyumba za walimu pamoja na madarasa.

Pia, Rage alikabidhi pikipiki mbili kwa chama cha waendesha bodaboda na kuahidi kuendelea kutoa misaada mingine kadiri atakavyoweza.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa CCM Tabora Mjini, Moshi Nkonkota, alilitupia lawama Jeshi la Polisi, kuwa hawataki kulinda mikutano ya CCM na kusababisha wafanyiwe vurugu.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More