Dodoma/Arusha. Wakati maofisa wa Shirika la Upelelezi wa Marekani (FBI)
wametua Arusha, raia wanne wa Saudi Arabia na Watanzania wawili
wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika kulipua bomu lililoua watu wawili na
kujeruhi wengine 61 wakati wa ufunguzi wa Kanisa la Mtakatifu Joseph
Parokia ya Olasiti.
Waliofariki dunia ni Regina Longino Kurusei (45),
mkazi wa Olasiti na James Gabriel (16), ambaye alifariki usiku wa
kuamkia jana.
Tukio hilo lilitokea wakati Balozi wa Vatican na
Mwakilishi wa Papa nchini, Francisco Montecillo Padilla alipokuwa
akizindua kanisa hilo.
Akitoa maelezo kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
jana, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema raia hao wa Saudi
Arabia walikamatwa jana asubuhi baada ya tukio wakiwa kwenye gari
wakielekea Kenya kupitia Namanga.
Mulongo alisema raia hao wa kigeni
waliingia nchini Jumamosi iliyopita na siku iliyofuata ndipo kukatokea
ulipuaji huo. Alisema lengo la shambulizi hilo lilikuwa kumdhuru Askofu
Padilla.
“Mtu ambaye tulimkamata jana (juzi Jumapili) ndiye
aliyesaidia kuwapata watu hawa wa Saudi Arabia na Watanzania hao,”
alisema Mulongo.
Mulongo alisema maofisa wa FBI walifika jana saa
tano asubuhi ili kusaidiana na Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), katika uchunguzi wa tukio hilo.
Maofisa hao wa FBI walikuwa
Zanzibar ambako walikuwa wanachunguza kifo cha Padri Evaristus Mushi
ambaye aliuawa Februari 17, mwaka huu.
Hii itakuwa mara ya pili kwa
wageni kuhusishwa na matukio ya ugaidi nchini baada ya mwaka 1998 wakati
raia kadhaa wa Misri wakiongozwa Fazul Abdulla waliposhirikiana na
Watanzania kadhaa akiwamo Ahmed Ghailani kulipua ubalozi wa Marekani
nchini na ule wa Kenya. Ghailani anatumikia kifungo cha maisha nchini
Marekani wakati Fazul aliuawa Somalia mwaka 2011.
Tamko la Serikali
Akitoa
tamko la Serikali bungeni jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi alimtaja mmoja wa watuhumiwa wanaoshikiliwa kuhusika na
tukio hilo kuwa ni Victor Calisti Ambrose (20), mkazi wa Kwa Mrombo
Arusha ambaye ni dereva wa bodaboda. Alisema kijana huyo ndiye
anayetuhumiwa kurusha bomu hilo.
Waziri Nchimbi alitoa onyo kali kwa
wanasiasa wanaopandikiza chuki za kidini miongoni mwa Watanzania na
kuishutumu Serikali kutokana na matukio kama hayo. “Kuna wanasiasa ambao
wanaona masilahi yao ni muhimu kuliko maisha ya Watanzania, masilahi
yao ni muhimu kuliko utulivu wa Watanzania na masilahi yao ni muhimu
kuliko umoja wa Watanzania.”
JK akatiza ziara, Bilal atoa ahadi
Rais
Jakaya Kikwete, amekatiza ziara yake ya kiserikali nchini Kuwait ili
kurejea nyumbani kutokana na shambulio la bomu kwenye kanisa hilo.
Taarifa
ya Ikulu imesema jana kwamba Rais Kikwete amelazimika kukatiza ziara
hiyo na kurejea nyumbani mara moja ili kuwa karibu na wafiwa pamoja na
wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.
Makamu wa Rais,
Dk Gharib Bilal ameahidi kuwa Serikali itahakikisha wote waliohusika na
tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.
Balozi wa Papa atoa tamko
Askofu
Padilla ambaye jana alitembelea majeruhi katika Hospitali ya Mkoa,
Mount Meru, alieleza kustushwa na tukio hilo na kusema hakutarajia kitu
kama hicho kutokea wakati wa shughuli hiyo wakati Watanzania
wakijulikana ni watu wa amani.
Alilaani tukio hilo na kuvitaka vyombo vya usalama kufanya uchunguzi ili kubaini ukweli.
Kanisa Katoliki Arusha
Kanisa
Katoliki, Jimbo Kuu la Arusha jana liliitaka Serikali iwataje
waliohusika na tukio hilo la kigaidi huku likiwataka waumini wake
kutolipiza kisasi.
“Msimamo wa kanisa katika hili, ni kuwataka
waumini wasilipize kisasi kama ambavyo alisema Yesu Kristo kuwa
msilipize kisasi, muwe tayari kushinda ubaya kwa wema,” alisema Askofu
Josephat Lebulu na kuongeza:
EU
Jumuiya ya Umoja wa Ulaya
(EU), imetaka kuharakishwa kwa uchunguzi wa tukio hilo na kuonya kuwa
matukio kama hayo yanaweza kulitumbukiza taifa kwenye machafuko.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Balozi wa Umoja huo nchini,
Filiberto Ceriani-Sebregondi alisema Tanzania inapaswa kufahamu kwamba
pasipo kujenga, kuendeleza na kusisitiza utamaduni wa kuvumiliana, hali
inaweza kuwa mbaya zaidi kwa siku za usoni.
0 maoni:
Chapisha Maoni