Dodoma. Serikali imesema mpango wa kufanya doria za anga katika Mlima Kilimanjaro kwa kutumia helkopta, haujapata mafanikio kutokana na hali ya hewa pamoja na mazingira ya mlima huo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu, alisema hayo jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalumu, Betty Machangu, aliyeuliza kwa nini Serikali isitumie helkopta
katika doria zake kwenye mlima huo lengo likiwa ni kuwadhibiti wahalifu.
Katika majibu yake, Nyalandu alisema kutokana na
mlima huo kuwa na msitu mnene uliofunga na kuuzunguka mlima huo,
miteremko, makorongo na mito iliyopo inakuwa vigumu kuona wahalifu walio
chini kama doria za helkopta zikitumika.
“Doria nyingi zinazofanyika katika mlima huo
hufanywa kwa miguu ambapo magari hupeleka askari jirani na maeneo
tarajiwa ya doria. Doria hizo zimekuwa na mafanikio makubwa na imesaidia
sana kudhibiti uhalifu katika hifadhi,” alisema.
Alieleza kwamba, pamoja na doria hizo za miguu na
magari, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), litaendelea kutumia
helikopta katika kudhibiti uhalifu kwenye maeneo ya wazi katika hifadhi
ya Kilimanjaro na hifadhi zingine.
0 maoni:
Chapisha Maoni