Katika kesi hiyo, Li ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya China,
alikuwa akilalamikia hatua ya kuondolewa kwenye nyumba Nambari 103
iliyopo katika vitalu namba 3, 5, 7 na 8, Barabara ya Haile Selassie,
Oysterbay, Dar es Salaam.
Kesi dhidi ya NHC ilifunguliwa mwaka 2006 wakati
shirika hilo likiongozwa na Martin Madekwe na imedumu kwa miaka sita
hadi Aprili mwaka jana ilipotolewa hukumu wakati shirika hilo likiwa
chini ya Nehemia Mchechu aliyeteuliwa mwaka 2010.
Katika hukumu yake ya Aprili 27, 2012, Jaji Atuganile Ngwala aliamuru NHC pamoja na washtakiwa wa pili na wa tatu katika shauri hilo; Lars Eric Hulstrom na Kampuni ya Udalali ya Manyoni, wamlipe Li karibu Sh478 milioni ikiwa ni fidia ya hasara na usumbufu uliosababishwa na kuhamishwa kwake kinyume cha sheria katika nyumba hiyo.
Mchanganuo huo unahusisha Sh70 milioni na Dola za
Marekani 177,450 (Sawa na Sh283, 920,000 - Dola moja ni sawa na
Sh1,600), gharama za kesi pamoja na riba ambazo pia zinapaswa kulipwa.
Pia Mahakama hiyo iliamuru Li arejeshwe katika
makazi hayo, amri ambayo inamaanisha kuondolewa katika nyumba hiyo kwa
mpangaji aliyeingizwa badala ya Li ambaye ni Hulstrom aliyekuwa mdaiwa
wa pili katika kesi hiyo.
Baada ya kupokea nakala ya hukumu ya Jaji Ngwala,
NHC waliazimia kukata rufaa kupinga uamuzi huo lakini habari kutoka
ndani ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi zinadai kwamba
Waziri Tibaijuka alitoa maelekezo ya mdomo kwamba hakukuwa na haja kwa
shirika hilo kukata rufaa.
Habari ambazo gazeti hili lilizipata zinadai
kwamba Waziri Tibaijuka aliitisha vikao kadhaa vilivyowahusisha
watendaji wa wizara yake na wale wa NHC na moja ya ajenda ilikuwa ni
kuwataka watendaji wa shirika hilo kuandaa taratibu za malipo na
utekelezaji wa amri nyingine za Mahakama na si vinginevyo.
Mwandishi wetu alifanikiwa kuona muhtasari wa
kikao cha Mei 21, 2012 jana ambazo zinamnukuu Profesa Tibaijuka
akiwaelekeza NHC kutokata rufaa dhidi ya uamuzi wa Mahakama na badala
yake wamlipe Li kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo, NHC kabla ya kutekeleza maelekezo ya
bosi wao huyo, iliomba ushauri wa kitaalamu kutoka Kampuni ya Uwakili;
Chuwa Advocates & Co., ambayo ilishauri kwamba kulikuwa na haja ya
kuukatia rufaa uamuzi huo wa Mahakama ushauri ambao mbali na kukubaliwa
na menejimenti pia ulipata baraka za bodi ya shirika hilo.
NHC kupitia Chuwa Advocates & Co. ilikata
rufaa katika Mahakama ya Rufani Tanzania Mei 29, 2012 ikipinga hukumu
hiyo katika kesi ya madai namba 71 ya 2012 ambayo mpaka sasa inaendelea
kusikilizwa na majaji watatu.
Uamuzi huo wa NHC unaelezwa kuwa umesababisha
mkwaruzano baina ya Waziri Tibaijuka na Mchechu.Alipoulizwa kuhusu madai
hayo, Mchechu alikiri kwamba kesi baina ya NHC na Li inaendelea
mahakamani lakini alikanusha kuwapo kwa mgogoro baina ya shirika
analoliongoza na Waziri Tibaijuka.Kwa upande wake, Waziri Tibaijuka
akizungumza mjini Dodoma alisema ni kweli kwamba kesi hiyo ipo
mahakamani na kusema hawezi kuilazimisha NHC kutekeleza suala ambalo
halijatolewa uamuzi wa kimahakama.
“Nadhani tuiachie Mahakama ifanye kazi yake na
uamuzi utakapotoka basi tutaona jinsi utekelezaji wake utakavyokuwa,”
alisema Profesa Tibaijuka.
0 maoni:
Chapisha Maoni