Alhamisi, 8 Agosti 2013

Bilionea Wama dini Mererani auawa kwa risasi 20 Moshi







Moshi. Mfanyabiashara tajiri wa Mirerani na Jijini Arusha, Erasto Msuya, ameuawa kwa kupigwa risasi zaidi ya 20 kwa kutumia bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG), jana mchana.
Erasto anayemiliki vitega uchumi kadhaa na anayeaminika kuwa miongoni mwa wafanyabiashara wa Mirerani wanaoongoza kwa utajiri,
aliuawa jana saa 7:00 mchana wilayani Hai mkoani Kilimanjaro.
“Eneo la tukio kumeokotwa maganda karibu 21 ya risasi zinazoaminika ni za SMG, yaani mwili ni matobo kila sehemu kwa kweli ameuawa kinyama sana,” alisema polisi mmoja wa Kituo cha Bomang’ombe.
Kufuatia mauaji hayo yaliyotokea kati ya neo la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na mji wa Bomang’ombe, mji huo ulifurika magari ya wachimbaji kutoka Moshi, Arusha na Mererani.
Habari za uhakika zilieleza kuwa wauaji wake walikuwa katika pikipiki na baada ya kumminia risasi hizo, walimpora kibegi ambacho haikujulikana kama kilikuwa na madini ama mamilioni ya fedha.
Kulingana na vyanzo vya habari, mfanyabiashara huyo alipigiwa simu na kukubaliana kukutana katikati ya mji wa Bomang’ombe na makutano ya Barabara ya Kia katika Barabara Kuu ya Hai kwenda Arusha.
RPC Kilimanjaro afafanua alivyouawa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alisema kuwa mfanyabiashara huyo aliuawa saa 7:00 mchana eneo la Mjohoroni kati ya mji wa Bomang’ombe na makutano ya barabara ya Kia.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Eransto alikuwa akitokea Moshi kuelekea Arusha, na alipofika hilo eneo la Mjohoroni alichepuka na kwenda meta 300 nje ya barabara,” alisema.
Kamanda Boaz alisema alipofika eneo hilo, alikutana na vijana wawili waliokuwa na pikipiki ambao waliingia ndani ya gari kwa lengo la kufanya mazungumzo yanayodhaniwa ni ya kibiashara.
Hata hivyo, muda mfupi tu Erasto alishuka kwenye gari lake na kuanza kukimbia na ndipo mmoja kati ya wale vijana alishuka kwenye gari la Erasto na kuanza kumminia risasi nyingi.
Kijana pekee wa kabila la kimasai anayedaiwa kushuhudia mauaji hayo, aliwaeleza polisi kuwa mara baada ya Erasto kufika eneo hilo la mtaa wa Wasomali, alisimamisha gari na kuwapigia wauaji.
Habari hizo zimedai kuwa vijana wale wawili walipokea simu hiyo na kumtaka ashuke kwenye gari lake la kifahari aina ya Range Rover New Model, ili wafanye biashara ambayo haijui.
Inadaiwa kuwa Erasto alipojaribu kupeleka mkono ili achomoe bastola, mmoja wa wale vijana alianza kumshambulia kwa risasi nyingi ambazo zilimfanya afariki dunia papo hapo.
Kijana huyo wa kimasai anayedaiwa kuwa msaada mkubwa kwa polisi, alidai kuwa baada ya Erasto kudondoka chini, vijana hao walichukua begi alilokuwa nalo na kutokomea.
Pikipiki iliyotumika yapatikana
Taarifa zilizopatikana baadaye jana jioni zilisema pikipiki iliyotumika katika tukio hilo imepatikana katika kijiji cha Olkolili, huko Sanyajuu wilayani Siha mkoani Kilimanjaro.
Kamanda Boaz alithibitisha kupatikana kwa pikipiki hiyo yenye nambari za usajili T316 CLV ikiwa imetelekezwa baada ya gurudumu moja kupata pancha baada ya kufika katika eneo hilo.
“Kwa vile tulikuwa tumesambaza taarifa kila mahali kwamba kuna raia wema walituarifu kuwa kuna watu wametelekeza pikipiki, baada ya kupata pancha na walikuwa wakitembea kwa miguu,” alisema.
Alisema Polisi walikwenda katika eneo hilo na mashuhuda walioshuhudia tukio hilo la mauaji wameitambua pikipiki hiyo kuwa ndiyo iliyokuwa ikitumiwa na wauaji wa mfanyabiashara huyo.
Kamanda Boaz alisema pia kuwa polisi watachunguza kwa kina mawasiliano ya simu ya mfanyabiashara huyo, kwa lengo la kutafuta watu wa mwisho kuwasiliana na marehemu.

Utajiri wake marehemu Msuya Katika kipindi cha uhai wake, marehemu alikuwa akijihusisha na uchimbaji na biashara ya madini ya Tanzanite katika mji mdogo wa Mirerani na jiji la Arusha. Kutokana na biashara zake hizo, alimudu kumiliki mali kadhaa zikiwemo nyumba za kawaida za kuishi pamoja na hoteli maarufu Arusha ya SG Resort iliyoko eneo la Sakina. Pamoja na hoteli na nyumba kadhaa zilizoko mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, marehemu pia alikuwa akimiliki magari kadhaa ya kifahari. Nyongeza na Peter Saramba, Arusha

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More