Brazil. Timu ya taifa ya Brazil
juzi imeichapa Italia 4-2 katika mashindano ya Kombe la Mabara na hivyo
Brazil kumaliza hatua ya makundi ikiongoza kundi A.
Mshambuliaji Neymar wa Brazil katika mechi hiyo alifunga bao na hivyo kufikisha mabao matatu katika mashindano hayo.
Brazil ilipata bao la kwanza mwishoni mwa kipindi
cha kwanza ambalo lilifungwa na Dante, lakini Italia ilisawazisha bao
hilo katika dakika ya 51 mfungaji akiwa Emanuele Giaccherini.
Katika dakika ya 55, Neymar aliifungia Brazil bao
la pili baada ya kupiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja nyavuni
na kumuacha kipa mahiri wa Italia, Gianluigi Buffon asijue la kufanya.
kama hiyo haitoshi Brazil ilipata bao la tatu
katika dakika ya 66 ambalo lilifungwa na Fred, lakini Italia nao
hawakubaki nyuma kwani katika dakika 71 walifunga bao la pili ambalo
lilifungwa na Giorgio Chiellini.
Katika dakika ya 80 bado kidogo Italia
wangesawazisha hata hivyo mpira wa kichwa uliopigwa na Christian Maggio
ulipita juu kidogo ya goli. Pia dakika chache baadaye Mario Balotelli
naye alipiga shuti kali, lakini lilitoka nje.
Ilipofika dakika ya 89, Brazil ilijihakikishia
ushindi wa mechi hiyo kwani Fred alitumia vizuri mpira uliopanguliwa na
kipa wa Italia na hivyo kuiandikia Brazil bao la nne.
Brazil imemamaliza hatua hii ya makundi ikiwa na
pointi tisa ikiwa na pointi tatu juu ya Italia inayomfuatia huku timu za
Mexico na Japan zikitolewa mashindanoni.
“Brazil ipo tayari kwa ajili ya mechi ya nusu
fainali, tumefanikiwa kusonga mbele kwa sababu ya ufundi mzuri na mbinu
bora, pia kikosi kinajiamini,”alisema kocha wa Brazil, Luiz Felipe
Scolari.
0 maoni:
Chapisha Maoni