SIKU chache baada ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta, kutangaza timu inayoundwa na kundi lake kuwania urais
2015, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis
Mgeja, amesema chama hicho kinatakiwa kumchukulia hatua za kinidhamu kwa
sababu anahatarisha uhai wa chama.
Alisema, kama chama kitamuacha aendelee kutoa kauli
zinazohatarisha uhai wa chama, CCM itajiweka katika mazingira mabaya
kisiasa pindi wapinzani watakapoanza kuchambua kauli hizo.
Kauli
hiyo ya Mgeja, aliyoitoa jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza
na waandishi wa habari, imekuja ikiwa ni siku chache tu tangu Sitta
aitaje timu inayoundwa na kundi lake kuwania ukuu wa dola mwaka 2015.
Alisema
wanaounda timu hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, ambaye hata hivyo amekana kuwamo
kwenye timu hiyo.
Jana akimzungumzia Sitta, Mwenyekiti huyo wa
CCM, Mgeja alimshushia tuhuma nyingi akimwita mkorofi, mlalamishi na
kwamba anaonekana wazi kukihujumu chama.
Mgeja pamoja na mambo
mengine, alimshutumu Sitta kuwa alianzisha CCJ akiwa ndani ya CCM, kisha
akataka kuhamia Chadema akiwa ndani ya CCM na yote hayo chama kiliyajua
na kumwacha.
Alisema Sitta yeye ni waziri, lakini kuna wakati
alikaririwa akisema kwamba, Serikali iwaombe radhi wananchi kwa sababu
ya mgawo wa umeme, baadaye akasema maisha bora kwa kila Mtanzania
hayawezekani na sasa amekaririwa hivi karibuni akisema Rais Kikwete
alimhujumu kwenye uspika.
“Yaani anajiamini kiasi cha kuanza
kumchokonoa hata Rais Kikwete, wakati akijua kwamba mambo anayoyafanya
yanakwenda kinyume na mtazamo wa chama.
“Hivi huyu ni mtu gani
asiyetosheka, kila wakati analalamika wakati yeye ni waziri na ana
nafasi kubwa ya kupeleka malalamiko yake kwenye chama ili yakafanyiwe
kazi.”
Alisema kama Sitta anaona yuko kwenye basi lenye abiria
asioendana basi aondoke na kuhoji anafanya nini ndani ya CCM wakati
anaonekana wazi kwamba haridhishwi na mwenendo wa chama na Serikali.
Mgeja
pia alimtaka Sitta kwenda TAKUKURU kama anaona kuna rushwa ndani ya
chama, au kama kuna wezi aende polisi na kama anaona kuna wahalifu, basi
aende mahakamani.
“Lakini huyu mzee lazima chama kimchukulie
hatua, huyu ni mzigo, kama hatadhibitiwa atakiharibu chama kwa sababu
anaonekana ana ajenda ya siri,” alisema.
Mgeja aliitaka Kamati ya
Maadili ya chama inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho,
Philip Mangula, imjadili ili ijulikane ana ajenda gani.
Alisema kwa upande wake katika kikao cha NEC kijacho, atawasilisha hoja binafsi kutaka Sitta ajadiliwe.
“Yeye
anajifanya ni msafi wakati mambo yake mengi tunayo, kwani hata
alipopata uspika anaouota hadi sasa, alibebwa, tena kwa kampeni kali
kweli kweli. Hivi, kwa nini asiwe kama mzee Msekwa (Pius Msekwa) ambaye
baada ya kushindwa uspika alinyamaza kimya?” alifoka Mgeja.
Kwa
mujibu wa Mgeja, kitendo kinachofanywa na Sitta ni cha hatari kwa uhai
wa chama na kwamba kama isingekuwa huruma ya Mwenyekiti wa CCM, Taifa,
Rais Jakaya Kikwete, angeshafukuzwa uanachama wa CCM.
“Kuna
wakati tulikaa tukataka kumnyang’anya kadi na aliokolewa na Mwenyekiti
wetu, lakini pamoja na kusamehewa, bado hatulii, anaendeleza mambo yake
ya ajabu ajabu,” alisema.
Akizungumzia kauli ya Sitta ya wiki hii
aliyoitoa akiwataja Magufuli, Membe na Dk. Mwakyembe kwamba ni wasafi,
alisema ni ya kibaguzi, kwa kuwa waliotajwa ni Wakristo, wala hakuna
Muislamu hata mmoja.
“Aliowataja wote hao akiwa kanisani ni
wakristo, wala hakuna Muislamu, wote hao ni wanaume na hakuna mwanamke,
pia hao wote ni kutoka Tanzania Bara na inavyoonekana Unguja na Pemba
hakuna watu safi.
“Sasa mtu kama anadiriki kusema uongo, tena
madhabahuni, ana sifa gani ya kuwa kiongozi, yaani amefika mahali sasa
anaanza ubaguzi wa Watanzania Bara na Visiwani, anaanza kubagua jinsia,
huyu hafai na lazima achukuliwe hatua.
“Namtaka anyamaze,
asiendelee na mambo yake kwa sababu kama ataendelea kupiga porojo,
nitasema mengi zaidi yanayomhusu kwa sababu siyo msafi kama anavyotaka
kuwadanganya Watanzania,” alisema.