Jumapili, 2 Juni 2013

Mgeja ataka Sitta afukuzwe CCM kwa usaliti


SIKU chache baada ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, kutangaza timu inayoundwa na kundi lake kuwania urais 2015, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, amesema chama hicho kinatakiwa kumchukulia hatua za kinidhamu kwa sababu anahatarisha uhai wa chama.

Alisema, kama chama kitamuacha aendelee kutoa kauli zinazohatarisha uhai wa chama, CCM itajiweka katika mazingira mabaya kisiasa pindi wapinzani watakapoanza kuchambua kauli hizo.

Kauli hiyo ya Mgeja, aliyoitoa jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari, imekuja ikiwa ni siku chache tu tangu Sitta aitaje timu inayoundwa na kundi lake kuwania ukuu wa dola mwaka 2015.

Alisema wanaounda timu hiyo ni pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, ambaye hata hivyo amekana kuwamo kwenye timu hiyo.

Jana akimzungumzia Sitta, Mwenyekiti huyo wa CCM, Mgeja alimshushia tuhuma nyingi akimwita mkorofi, mlalamishi na kwamba anaonekana wazi kukihujumu chama.

Mgeja pamoja na mambo mengine, alimshutumu Sitta kuwa alianzisha CCJ akiwa ndani ya CCM, kisha akataka kuhamia Chadema akiwa ndani ya CCM na yote hayo chama kiliyajua na kumwacha.

Alisema Sitta yeye ni waziri, lakini kuna wakati alikaririwa akisema kwamba, Serikali iwaombe radhi wananchi kwa sababu ya mgawo wa umeme, baadaye akasema maisha bora kwa kila Mtanzania hayawezekani na sasa amekaririwa hivi karibuni akisema Rais Kikwete alimhujumu kwenye uspika.

“Yaani anajiamini kiasi cha kuanza kumchokonoa hata Rais Kikwete, wakati akijua kwamba mambo anayoyafanya yanakwenda kinyume na mtazamo wa chama.

“Hivi huyu ni mtu gani asiyetosheka, kila wakati analalamika wakati yeye ni waziri na ana nafasi kubwa ya kupeleka malalamiko yake kwenye chama ili yakafanyiwe kazi.”

Alisema kama Sitta anaona yuko kwenye basi lenye abiria asioendana basi aondoke na kuhoji anafanya nini ndani ya CCM wakati anaonekana wazi kwamba haridhishwi na mwenendo wa chama na Serikali.

Mgeja pia alimtaka Sitta kwenda TAKUKURU kama anaona kuna rushwa ndani ya chama, au kama kuna wezi aende polisi na kama anaona kuna wahalifu, basi aende mahakamani.

“Lakini huyu mzee lazima chama kimchukulie hatua, huyu ni mzigo, kama hatadhibitiwa atakiharibu chama kwa sababu anaonekana ana ajenda ya siri,” alisema.

Mgeja aliitaka Kamati ya Maadili ya chama inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula, imjadili ili ijulikane ana ajenda gani.

Alisema kwa upande wake katika kikao cha NEC kijacho, atawasilisha hoja binafsi kutaka Sitta ajadiliwe.

“Yeye anajifanya ni msafi wakati mambo yake mengi tunayo, kwani hata alipopata uspika anaouota hadi sasa, alibebwa, tena kwa kampeni kali kweli kweli. Hivi, kwa nini asiwe kama mzee Msekwa (Pius Msekwa) ambaye baada ya kushindwa uspika alinyamaza kimya?” alifoka Mgeja.

Kwa mujibu wa Mgeja, kitendo kinachofanywa na Sitta ni cha hatari kwa uhai wa chama na kwamba kama isingekuwa huruma ya Mwenyekiti wa CCM, Taifa, Rais Jakaya Kikwete, angeshafukuzwa uanachama wa CCM.

“Kuna wakati tulikaa tukataka kumnyang’anya kadi na aliokolewa na Mwenyekiti wetu, lakini pamoja na kusamehewa, bado hatulii, anaendeleza mambo yake ya ajabu ajabu,” alisema.

Akizungumzia kauli ya Sitta ya wiki hii aliyoitoa akiwataja Magufuli, Membe na Dk. Mwakyembe kwamba ni wasafi, alisema ni ya kibaguzi, kwa kuwa waliotajwa ni Wakristo, wala hakuna Muislamu hata mmoja.

“Aliowataja wote hao akiwa kanisani ni wakristo, wala hakuna Muislamu, wote hao ni wanaume na hakuna mwanamke, pia hao wote ni kutoka Tanzania Bara na inavyoonekana Unguja na Pemba hakuna watu safi.

“Sasa mtu kama anadiriki kusema uongo, tena madhabahuni, ana sifa gani ya kuwa kiongozi, yaani amefika mahali sasa anaanza ubaguzi wa Watanzania Bara na Visiwani, anaanza kubagua jinsia, huyu hafai na lazima achukuliwe hatua.

“Namtaka anyamaze, asiendelee na mambo yake kwa sababu kama ataendelea kupiga porojo, nitasema mengi zaidi yanayomhusu kwa sababu siyo msafi kama anavyotaka kuwadanganya Watanzania,” alisema.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More