Jumatano, 12 Juni 2013

TFDA: Kiwanda cha TPI kilisambaza ARV feki kwa Watanzania


MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA), imethibitisha dawa bandia za kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (ARV), zilitengenezwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industry (TPI). Taarifa hiyo, ilitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Hiiti Sillo, wakati wa semina kwa wabunge iliyoandaliwa na Bohari ya Dawa (MSD).

Sillo, alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), aliyetaka kujua kama dawa hizo bandia za ARV kweli zilitengenezwa na kiwanda cha TPI.

“Ninyi TFDA, mlikuwa wapi hadi kiwanda hicho kinazalisha dawa bandia za ARV?” alihoji Machali.

Alisema ni kweli dawa hizo bandia, ziligundulika zikiwa tarari zipo sokoni katika hospitali mbalimbali, ikiwemo Hospitali ya Tarime mkoani Mara.

“TDFA ilifanya uchunguzi wa kitaalamu na kubaini dawa hizo ni bandia na baada ya uchunguzi pia na kwa mujibu wa nyaraka, ilibainika dawa hizo zilitengenezwa na Kiwanda cha TPI ambayo ndiyo iliyoisambazia dawa hizo MSD,” alisema Sillo.

Mbunge wa Njombe Kaskazini, Deo Sanga (CCM), aliitaka Serikali kupeleka muswada bungeni kutunga sheria kali kwa watakaobainika kuuza dawa za Serikali katika maduka binafsi.

“Sheria hii kali ikitungwa, dawa za Serikali hazitakutwa kwenye maduka binafsi na zikikutwa zitaifishwe,” alisema.

Awali akifungua semina hiyo, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, alisema lengo la semina hiyo ni kushirikishana uzoefu na wabunge juu ya mfumo wa usambazaji dawa nchini.

Alisema semina hiyo, ilikuwa na mada nne, ikiwemo hiyo ya mfumo wa usambazaji wa dawa na vifaa tiba wa Bohari ya Dawa, ikiwemo kuzungumzia mikakati mbalimbali ya kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa dawa katika vituo vya kutolea huduma.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa MSD, Cosmas Mwaifwani, alisema mbali na jitihada mbalimbali zinazofanywa na bohari hiyo, aliwaomba wateja wake kuboresha mfumo wa utunzaji kumbukumbuku katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote.

“Kuongeza usimamizi wa dawa na vifaa tiba ngazi ya wilaya, kupitia Kamati za Afya za Wilaya ili kuboresha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vituoni,” alisema.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More