Jumanne, 16 Aprili 2013

CD Za zinazochochea Udini zatinga Bungeni


MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA) amewasilisha CD za video alizodai kuwa ni za uchochezi wa kidini na kutaka serikali ichukue hatua.
Mbunge huyo alitumia nafasi hiyo jana wakati akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Selasini alisema CD hizo moja ni ya wanachuo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), wakiwa na wahadhiri wao wa dini moja, wakitoa maneno ya uchochezi na kupanga namna ya kuwashughulikia wanachuo wenzao wa dini nyingine ambao wanaishi nao kwenye bweni moja.
Alisema CD nyingine inaonesha kiongozi mmoja wa dini akitoa kauli za kutaka  maaskofu, mapadri na viongozi wengine wa Kikristo wauawe.
”CD hizo zinajulikana, lakini serikali haijachukua hatua. Hii maana yake suala la ubaguzi wa kidini linachochewa na linahamasishwa na baadhi ya viongozi wa serikali na CCM,” alisema.
Selasini alisema hakuna sababu ya serikali kupoteza muda kukutana na viongozi wa dini za Kikristo na Kiislamu kujadili suala hilo la udini badala yake ichukue hatua kwa wachochezi hao.
Akitolea mfano, Selasini alisema mwaka 2005 aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Omari Mahita, alitangaza kukamata shehena ya kontena la visu na majambia, mali ya Chama cha Wananchi (CUF).
Selesini aliongeza kuwa licha ya CUF kuchafuliwa kwa tuhuma hizo ambazo hadi sasa hazikufikishwa mahakamani, chama hicho hakikuwahi kuombwa radhi wala Mahita hakuchukuliwa hatua zozote na serikali.
Pia alisema wapo waliotangaza kwamba CUF ni chama cha Kiislamu, CHADEMA ni chama cha Kikristo, Wachaga, lakini hakuna aliyechukua hatua kwa kauli hii ya kibaguzi.
"Hiyo kesi ya majambia ya CUF iko wapi na kama haipo, Mahita alichukuliwa hatua gani? Leo wapo viongozi wanatangaza CHADEMA ni chama cha Kichaga, mara cha kigaidi. Hao wanachukuliwa hatua gani?” alihoji Selasini.
Mbunge huyo alilalamikia vyombo vya dola kuwa vinaachia CD za uchochezi na badala yake vinachukua picha za video kwenye mitandao ya You tube na kuwabambikizia kesi watu wasio na hatia.
Wakati Selasini akilalamikia CD hizo ikiwemo ile aliyodai ni ya UDOM, Mbunge mwingine wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Juma Nkamia (Kondoa Kusini), alisema hali katika chuo hicho ni shwari na hakuna tatizo la udini.
”Hapa tunataka kuonesha kwamba UDOM kuna tatizo, si kweli. Kama tatizo ni baadhi ya maprofesa kwa sababu ya dini zao, basi waondolewe,” alisema Nkamia.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More