Jumatano, 24 Aprili 2013

MAMA ZITTO AVAMIWA NA WATU WALIOTAKA KUMUHUA

 







SHIDA Salum, mama mzazi wa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo 
(CHADEMA), Zitto Kabwe, amenusurika kuuawa baada ya kuvamiwa nyumbani kwake na watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, wakiwa na silaha za moto.
Habari zilizolifikia MTANZANIA Jumatano kutoka kwa watu walio karibu na mama huyo zilieleza kuwa, vijana hao walifanikiwa kumfikia akiwa katika sebule ya nyumbani kwake na kumuelekezea bastola kichwani, huku wakimlazimisha awakabidhi baadhi ya vifaa vyake vya kufanyia kazi na simu yake ya kiganjani.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, tukio hilo lilitokea Ijumaa ya Aprili 19, majira ya saa moja na nusu asubuhi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumatano kupitia simu yake ya kiganjani kuhusu tukio hilo, mama yake Zitto alisema ni kweli lilitokea na amekwisharipoti katika kituo cha Polisi cha Buguruni.

Mama Zitto alisema siku kadhaa kabla ya tukio hilo alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanachama wa Chadema wa Tawi la Tabata Relini na kumuomba msaada wa mifuko miwili ya saruji kwa ajili ya kukarabati jengo la ofisi yao.

Alisema alikubali kuwasaidia vijana hao kwa kuwataka wafike nyumbani kwake mapema siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita, kwa sababu alikuwa na ratiba ngumu na ndefu siku hiyo.

“Nilikubaliana nao hivyo, bila kuwa na fikra kwamba wanaweza kuwa watu wabaya, hivyo walipokuja nyumbani kwangu baada ya kuruhusiwa na mlinzi niliwakaribisha ndani na kuwaeleza kuwa nitawapatia Sh 20,000 na Sh10,000 waongeze wenyewe.

“Lakini niliposimama kuelekea chumbani kuwachukulia kiasi hicho cha fedha, mmoja wao alitoa bastola na kunielekezea kichwani huku akieleza kuwa hawana shida na pesa, bali wanataka laptop yangu, flash na simu yangu ya mkononi kwa sababu zina mambo muhimu,” alisema mama Zitto.

Alieleza zaidi kuwa alipowauliza ni kwa nini wanataka vitu vyake hivyo, walieleza kuwa anajua sababu na hata siri yake ya kutumia nafasi yake ya uongozi wa chama cha walemavu kuzunguka nchi nzima akimnadi mwanaye Zitto kwa wana Chadema kuwa anafaa kuwa mwenyekiti wa chama hicho na rais wa Tanzania inafahamika.

“Nilijua kuwa ninakufa, sikuona haja ya kubishana nao sana, nikamwita dereva wangu, Mtana, alete simu yangu niliyokuwa nikiichaji chumbani na flash ili niwapatie, wakati akielekea kuvichukua aliwaona walivyokuwa wameniwekea bastola, akakimbia moja kwa moja chumbani akajifungia na kuanza kupiga kelele, wakatoka haraka wakakimbia,” alisema.

Alipoulizwa iwapo hawakupata upinzani wowote kutoka kwa mlinzi aliyekuwa getini au majirani walishtushwa na kelele za dereva wake, alisema wakati wanatoka geti lilikuwa wazi na mlinzi alikuwa akiosha gari nje, hivyo ilikuwa rahisi kutoka na gari lao na kutokomea.

Alisema anaweza kuwatambua watu hao akiwaona na kwamba mmoja wao si mgeni machoni mwake, kwa sababu aliwahi kumuona mkoani Tanga katika moja shughuli za chama hicho.

Mama Zitto alieleza zaidi kuwa kabla ya tukio hilo, amekuwa akiulizwa na baadhi ya wafuasi wa chama na hata watu wengine mahali anakopata fedha za kuzunguka mikoani kumnadi mwanaye, Zitto kwa ajili ya kugombea urais na uenyekiti wa chama.

Alisema kwa sababu ya kuhofia maswali ambayo amekuwa akiulizwa mara kwa mara, alimfikishia taarifa Kaimu Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Ahmed Sagula, lakini katika hatua ambayo hakuitegemea, naye alimhoji mahali anakopata fedha za kuzunguka mikoani kumnadi Zitto, kabla ya kumuahidi kushughulikia malalamiko yake.

Sagula mwenyewe hakuweza kupatikana jana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake kutopatikana kila ilipopigwa.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, naye hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo na hata Mkuu wa Kituo cha Polisi Buguruni, mahali ambako Mama Zitto ameripoti tukio hilo naye hakuweza kupatikana.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More