Alhamisi, 25 Aprili 2013

KUELEKEA UCHAGUZI 2015 MBINU MPYA HADHARANI BAINA YA KAMBI HASIMU

 



















ATIKA hali inayooshesha kupamba moto kwa harakati za kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), makundi ndani ya chama hicho yameanza kuungana.
Mbali ya kuungana kwa makundi, pia wale wote wanaotajwa kuwania kuteuliwa, macho na nyoyo zao vimeelekezwa kwa Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete, ambaye nguvu aliyonayo ndani ya vikao vya uteuzi inatarajiwa kutumika kumpata mgombea urais.
Ingawaje viongozi wa juu wa CCM wamekuwa wakipinga mjadala kuhusu mgombea urais au Rais ajaye ndani ya chama hicho kikongwe nchini, lakini mjadala huo unatajwa kufunika hata ile mijadala muhimu kwa maendeleo ya nchi.
Uchunguzi wa Rai umebaini kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ameanza ‘kurudisha majeshi’, na anatajwa kumuunga mkono Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ambaye anatajwa kuwa ‘safi’, mtu asiye na kikwazo mbele ya Rais Kikwete.

“Hali inavyoonekana sasa, Membe anaelekea kuungana na kambi ya Dk. Nchimbi, na si yeye pekee, wale wote ambao wanampinga Lowassa lakini wanajua hawana kura ndani ya CCM, wanaanza kumuunga mkono Nchimbi.

“Lengo kubwa hapa ni kutengeneza mgombea mmoja mwenye nguvu kubwa ili kumkabili Lowassa ambaye anatajwa kuwa na nguvu kubwa zaidi ndani ya chama katika ngazi zote.

“Katika hao, yumo Waziri Samuel Sitta, Dk. Harrison Mwakyembe na watu wao, lakini vile vile wanasahau uhusiano mzuri na kuheshimiana kati ya Lowassa na Dk. Nchimbi.

“Pia tetesi za kuwapo mpango wa kulikata jina la Lowassa katika ngazi ya Kamati Kuu lisirudishwe kwenye Mkutano Mkuu ambako anadaiwa kukubalika kuliko wagombea wengine, kunatajwa kuwa moja ya sababu za makundi kuungana,” alisema mchambuzi mmoja wa mambo ya siasa nchini.

Mgombea mwingine anayetajwa kupewa nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM 2015, ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira, ambaye tofauti na wagombea wengine, yeye hana kundi wala makundi.

Kutokana na kutokuwa na makundi, wachunguzi wa mambo wanasema haitakuwa rahisi jina lake kukwama katika ngazi ya Kamati Kuu, hivyo uwezekano wa jina lake kupigiwa kura na wajumbe wa Mkutano Mkuu kuchuana na wagombea wengine ni mkubwa.

“Huyu Mzee ana advantage moja kubwa, Kanda ya Ziwa inatajwa kuwa na idadi kubwa ya wapiga kura tofauti na maeneo mengi, na ni katika kanda hiyo hiyo Lowassa anaungwa mkono sana.

“Kama CCM wataamua kulikata jina la Lowassa, kuna uwezekano mkubwa sana kwa wana-CCM waliokuwa wakimuunga mkono kuhamishia kura zao kwa Wasira, na kumchagua,” alisema mchambuzi huyo.

Wakati hali ikiwa hivyo, pia imethibitika vigogo wa chama hicho wakiwamo wale wa kundi la wanamtandao lililomwingiza Rais Kikwete madarakani mwaka 2005 hawaaminiani katika harakati za kugombea urais kupitia CCM.

Uchunguzi unaonyesha vigogo wa CCM kutoka kambi zote wamekuwa wakiendesha kampeni za chini kwa chini kwa ajili ya kujiimarisha na kisha kuweza kuteuliwa kugombea kupitia chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu 2015.

Taarifa zinaonyesha kwamba hata baadhi ya vigogo wanaosadikiwa kuwa kundi moja sasa hawaaminiani jambo ambalo linaashiria kuwa vita ya urais CCM inapamba moto siku hadi siku.

Wakati wa vikao vyake vya juu vilivyomalizika Novemba 24 mwaka jana mjini Dodoma, CCM kilipokea na kupitisha taarifa ya hali ya siasa ambayo kimsingi ilibainisha kuwa hali ya siasa ndani ya chama si shwari, kutokana baadhi ya viongozi kupigana vikumbo kuwania madaraka.

Katika taarifa hiyo, CCM kilisema chanzo kikubwa cha migawanyiko ndani ya chama hicho ni harakati za kugombea urais mwaka 2015.

Hata hivyo, wimbi hilo la urais limeendelea kutikisa kambi ya wanamtandao ambayo taarifa za ndani zinasema huenda suala la urais likaibua mtafaruku mkubwa siku zijazo, hivyo kutoa mwanya kwa kundi jingine kuibuka kidedea.

“Kuna hali ya kutoaminiana ndani ya CCM, kila kundi sasa liko mstari wa mbele kujijega ili kuweza kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutoa mgombea urais.

“Hata ndani ya kundi la mtandao ambalo ndilo lenye nguvu kwa sasa wakubwa hawaaminiani,” alisema mtoa habari mmoja kutoka kundi la mmoja wa kiongozi anayetajwa kutaka kuwania urais ndani ya CCM.
Chanzo: gazeti la rai

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More